1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 40 watoweka baada ya boti ya wahamiaji kupinduka Italia

24 Juni 2023

Takriban watu 40 hawajulikani walipo baada ya boti ya wahamiaji kupinduka katika kisiwa cha Lampedusa nchini Italia.

https://p.dw.com/p/4T0gZ
Mittelmeer Boot mit Migranten in Seenot
Picha: Sea Watch/AP/picture alliance

Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi la UNHCR nchini Italia Chiara Cardoletti, amesema ajali hiyo ilitokea siku ya Alhamisi na mtoto mmoja mchanga ni miongoni mwa waliotoweka.

Msemaji wa shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM Flavio Giacomo, amesema boti hiyo iliondoka kutoka Sfax nchini Tunisia na ilikuwa imebeba wahamiaji 46 kutoka Cameroon, Burkina Faso na Ivory Coast.

Giacomo ameongeza kuwa boti hiyo ilipinduka kutokana na upepo mkali na mawimbi makubwa, na kwamba baadhi ya walionusurika walipelekwa Lampedusa huku wengine wakirudishwa Tunisia.

Miongoni mwa waliotoweka ni wanawake saba na mtoto mdogo. Watu wote walionusurika ni wanaume. Giacomo amesema pia kuwa tangu mwezi Novemba, wameshuhudia kuwasili kwa wahamiaji wengi kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara kupitia Tunisia.