1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafungwa 129 wauawa kufuatia jaribio la kutoroka jela Kongo

John Kanyunyu3 Septemba 2024

Siku moja baada ya wafungwa kwenye gereza kuu la mjini Kinshasa la Makala kujaribu kutoroka na baadhi kuuawa, serikali imetangaza matokeo ya mwanzo baada ya kuundwa tume kuchunguza tukio hilo.

https://p.dw.com/p/4kDVk
DR Kongo | Gereza la Makala mjini Kinshasa
Maafisa wa usalama wakishika doria mbele ya gereza la Makala mjini Kinshasa kufuatia jaribio la kutoroka jela.Picha: AP Photo/picture alliance

Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni waziri wa mambo ya ndani Jacquemin Shabani ametangaza matukio hayo usiku wa manane.

"Matokeo ya mwanzo kabisa ni kwamba kuna watu mia moja na ishirini na tisa waliouawa, na ishirini na nne kati yao waliuawa kwa risasi na wengine katika kugongana, kutokana na kukosa oxygen, na wanawake kadhaa walibakwa. Kamati ilihesabu majeruhi hamsini na tisa, wanaopatiwa matibabu na serikali. Kuna majengo ya utawala wa gereza yaliyochomwa moto, mukiwemo kituo cha afia, usajili wa mahakama na pia ghala ya vyakula. "

Navyo vyanzo vya habari huria vinasema,kwamba idadi ya wafungwa waliouawa wakati jeshi pamoja na polisi walijaribu kuwazuia wafungwa kutoroka, ni zaidi ya mia moja na ishirini na tisa kama ilivyotangazwa na serikali.

Soma pia: Watu 10 wauwawa katika shambulizi la kwenye baa mashariki mwa Congo 

Nalo shirika la kutetea haki za binaadamu Bill Clinton Fondation limetoa mwito wa  kufanyika uchunguzi huru, ili kujuwa ukweli wa kile kilichotokea kwenye gereza kuu la Makala.

DR Kongo | Gefangene arbeiten im Zentralgefängnis Makala in Kinshasa
Wafungwa wakiendelea na majukumu yao katika gereza kuu la Makala mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Str/Xinhua/picture alliance

Mratibu wa shirika hilo mjini Kinshasa Emmanuel Cole, analaani mauwaji ya wafungwa, huku akidai uchunguzi huru ufanyike.

"Palikuwa na mauwaji yaliyofanywa kwenye gereza na tunalikemea hilo. Na tunaomba uchunguzi wa kina ili serikali ya Congo ishitakiwe kwa kosa la kutowasaidia watu walieko kwenye hatari kwani, msiba huu ulipaswa kuhepukwa, serikali ingelichukuwa tahadhari."

Siku hizi hapa nchini Kongo, kunaripotiwa visa vingi vya mauwaji yanayotwikwa vyombo vya usalama katika maeneo mengi.

Soma pia: Kiongozi wa waasi Kongo ahukumiwa kifo

Patrick Mundeke, mshauri wa mpinzani Moïse Katumbi ametowa mwito wa kuanzishwa uchunguzi wa kimataifa, ili kuwatambuwa  na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wahusika kwa mauwaji ya raia katika matukio mbalimbali nchini Congo.

Ni alfajiri ya jana ndio milio ya silaha za kawaida na silaha nzito nzito ilisikika kwenye gereza kuu la Makala pamoja na viunga vyake, pale baadhi ya wafungwa walipokuwa wanajaribu kutoroka.

Mkasa wa Makala unatokea, wakati waziri wa sheria Constant Mutamba yupo katika harakati ya kuwaachia huru wafungwa kadhaa, ili magereza yaliyofurika wafungwa kupita kiasi, yapunguwe wafungwa.