1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watatu wafa kwenye mlipuko wa daraja la Crimea

9 Oktoba 2022

Urusi imesema watu watatu wamekufa katika mlipuko wa lori kwenye daraja linaloiunganisha na rasi ya Crimea. Mlipuko huo uliharibu daraja hilo la kilomita 19 wakati vita na Ukraine vikiwa vimepindukia miezi saba.

https://p.dw.com/p/4Hwc0
Schwere Schäden nach Explosion auf Krim-Brücke
Picha: AFP/Getty Images

Maafisa wa eneo hilo walisema hata hivyo daraja hilo lilifunguliwa na kuruhusu magari kupita lakini baada ya ukaguzi wa kina. Muda mfupi baadae, kampuni inayotoa huduma za reli ya Grand Service Express ilisema treni ya kwanza iliondoka kwenye rasi hiyo ya Crimea kuelekea Moscow na St. Petesburg.

Mlipuko huo umeibua minong'ono ya kwamba huenda Ukraine imehusika na kulipua daraja hilo wakati Moscow ikiwa haijataja moja kwa moja iwapo jirani yake huyo anahusika, na hata kwenye hotuba yake ya kila siku jioni, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky hakulizungumzia moja kwa moja suala hilo na maafisa hawakusema chochote kuhusiana na iwapo wamehusika na mlipuko huo.

Mapema jana picha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha daraja hilo likiwa linawaka moto na vipande vyake vikiangukia majini.

Wachunguzi wa Urusi wamesema watu watatu wamekufa. Maafisa hao pia waliiopoa kwenye maji miili ya mwanaume mmoja na mwanamke ambayo haikutambuliwa, ambayo wanasema huenda walikuwa ni abiria kwenye gari lilikuuwa karibu na eneo kulikotokea mlipuko huo.

Soma Zaidi: Shambulizi la Ukraine laua raia 7 Luhansk

Krim | Brand auf Kertsch-Brücke
Helikopta ikisaidia kuuzima moto kwenye matanki ya mafuta yaliyokuwa yanawaka baada ya mlipuko kwenye daraja hilo.Picha: REUTERS

Urusi aidha imesema wamemtambua mmiliki wa lori hilo ambaye ni raia wa mkoa wa Krasnodar ulioko kusini mwa Urusi na tayari walikuwa wakiipekua nyumba yake.

Ingawa rais Zelensky hakuzungumzia moja kwa moja mlipuko kwenye daraja hilo la kimkakati lakini mshauri wake Mykhailo Podolyak alichapisha picha ya sehemu ya daraja iliyoporomoka kupitia ukurasa wake wa twitter na kuandika "Crimea, daraja, ndio mwanzo". "Kila kitu ambacho si cha halali ni lazima kiharibiwe, kila kilichoibwa ni lazima kirudishwe Ukraine.." Lakini hata hivyo, baadae alionekana kuilaumu Urusi kuwa na mkono kwenye mlipuko huo.

Msemaji wa ikulu ya Urusi, Kremlin amesema rais Vladimir Putin tayari ameagiza kuundwa tume ya kuchunguza tukio hilo, wakati baadhi ya maafisa wakitoa mwito wa kulipizwa kisasi. Afisa aliyewekwa na Urusi katika jimbo ililolinyakua hivi karibuni la Kherson Kirill Stremousov amesem a "Kila mmoja anasubiri shambulizi la kulipiza kisasi, na hilo litafanyika."

Soma Zaidi: Putin asaini sheria inayohitimisha mchakato wa kuyanyakua maeneo ya Ukraine

Huku hayo yakiendelea, rais Zelensky wa Ukraine amesema jana jioni kwamba wanajeshi wake wako katika mapambano makali katika mji wake muhimu ulioko mashariki mwa nchi hiyo wa Bakhmut ambao Urusi inajaribu kuudhibiti.

Mara kadhaa vikosi vya Urusi vimejaribu kuukamata mji huo, uliopo kwenye barabara kuu inayoingia kwenye majiji ya Sloviansk na Kramatorsk. Majiji hayo yapo katika mkoa wenye viwanda wa Donbas ambao Moscow bado haijafanikiwa kuudhibiti kikamilifu.

Mashirika: AFP/RTRE