1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Eneo la makazi huko Zaporizhzhia lashambuliwa na Urusi

6 Oktoba 2022

Viongozi wa Ukraine wameitupia lawama Urusi kwa kufanya mashambulizi katika eneo la makazi karibu na kinu cha nyuklia za Zaporizhzhia.

https://p.dw.com/p/4HpTc
Ukraine | Raketenangriff auf Saporischschja
Picha: Marina Moiseyenko/AFP/Getty Images

Gavana wa Mkoa huo wa Ukraine ambao umedhibitiwa kwa kiasi kikubwa na Urusi amesema maroketi saba yalivurumishwa kwenye majengo karibu na Zaporizhzhia mapema leo alfajiri na kusababisha vifo vya watu wawili katika jiji hilo lililo karibu na kinu kikubwa zaidi cha nyuklia barani Ulaya.

Gavana Oleksandr Starukh ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Telegram kwamba watu wengi waliokolewa kutoka kwenye majengo ya ghorofa ikiwa ni pamoja na msichana wa miaka 3 ambaye alipelekwa hospitali kwa matibabu. Watu wengine watano haijulikani walipo.

Soma zaidi:Mkutano wa viongozi wa mataifa ya Ulaya mjini Prague kutuma ishara wazi kwa Urusi

Mashambulizi hayo yamejiri saa chache baada ya rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy kutangaza kwamba jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kuvikomboa vijiji vitatu katika mojawapo ya Mikoa iliyonyakuliwa kinyume cha sheria na Urusi.

 

IAEA kufanya mazungumzo na Ukraine

IAEA Direktor Rafael Grossi
Rafael Grossi, Mkuu wa IAEAPicha: Joe Klamar/AFP/Getty Images

Rafael Grossi, Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Nishati ya Atomiki - (IAEA) anatarajiwa wiki hii kufanya ziara mjini Kiev ili kujadili hali katika kituo cha Zaporizhzhia baada ya Rais wa Urusi Vladimir Putin kutia saini siku ya Jumatano agizo lililoweka wazi kwamba Urusi inachukua rasmi mamlaka katika kinu hicho cha nyuklia.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ukraine imesema hatua hiyo ya Urusi ni batili na pia ni kosa la jinai huku Shirika la Energoatom, limefahamisha kuwa litaendelea kuendesha shughuli katika mtambo huo.

Soma zaidi:Putin asaini sheria inayohitimisha mchakato wa kuyanyakua maeneo ya Ukraine 

Grossi, ambaye ataelekea pia mjini Moscow baada ya ziara yake mjini Kiev, atajadili pia na viongozi wa mataifa hayo mawili juhudi za kuandaa eneo salama na lenye ulinzi karibu na kituo cha Zaporizhzhia, ambacho kimeharibiwa katika mapigano hayo huku wafanyakazi wake akiwemo mkurugenzi mkuu wakitekwa nyara na askari wa Urusi.

Zelenskyy: Urusi tayari wameshindwa vita

Ukraine Präsident Zelenskiy
Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyyPicha: Valentyn Ogirenk/REUTERS

Katika hotuba yake ya usiku, Zelenskyy amewaambia viongozi wa Urusi kwamba tayari wameshindwa vita ambavyo walivianzisha Februari 24:

 

"Hatuna mashaka juu ya kuvishinda vita hivi na pia uwezo wetu wa kulinda uhuru wa Ukraine. Ushindi wa kila siku katika uwanja wa mapambano, pamoja na miji na vijiji vilivyokombolewa vinathibitisha hilo.  Swali letu ni moja tu: Ni raia wetu wangapi ambao Urusi itafaulu kuwaua na ni kiasi gani Urusi itaweza kuipora Ukraine kabla haijakubali kushindwa?

Soma zaidi:Baraza la juu la Bunge la Urusi laridhia unyakuzi wa majimbo manne ya Ukraine 

Urusi ilitwaa mikoa minne ya Ukraine wiki hii ukiwemo wa Zaporizhzhia licha ya kutokuwa na udhibiti kamili katika maeneo hayo. Ukraine imetangaza kuvikomboa vijiji vitatu kaskazini mashariki mwa Kherson na hivyo kulitia doa jeshi la Urusi ambalo limekuwa likijinadi kuwa na nguvu.