1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Warundi wanaoishi uhamishoni waombwa kurejea nyumbani

29 Novemba 2022

Serikali ya Burundi imewahakikishia Usalama na amani raia wake wanaoishi uhamishoni, Tanzania na kuwahimiza kurejea nyumbani baada ya kumaliza takribani miaka 7 uhamishoni.

https://p.dw.com/p/4KERl
Afrika DR Kongo Kayembe Camp
Picha: GUERCHOM NDEBO AFP via Getty Images

Hayo yamebainishwa katika kambi ya Nyarugusu inayohifadhi wakimbizi zaidi ya 40000 wa Burundi wakati viongozi wa Burundi na raia wake waliowahi kuwa wakimbizi wakitoa ushuhuda wa amani wa nchi yao kwa wakimbizi. Naibu Waziri wa Mambo ya ndani wa Jamhuri ya Burundi Bw. Nibona Bonansize Celestin amebainisha kuwa kwa sasa hakuna kitisho chochote cha kuwazuia wakimbizi kurejea Burundi.

soma zaidi:Wakimbizi wa Burundi Tanzania waahidiwa amani nyumbani

Kwa upande wake inspector Generali wa Polisi Burundi Ndihokubwayo Isidore amewahakikishia wakimbizi uwepo wa usalama wa kutosha ukilinganisha na wakati walipokimbia. Hata hivyo wakimbizi wenyewe licha ya kutaja kuwa na nia ya kurejea wameelezea hofu yao inayotokana na kitendo cha baadhi ya wanaorejea kurudi tena ukimbizini wakitaja kuwepo kwa vitisho.

Barubike Marie ni raia wa Burundi aliyewahi kuwa mkimbizi na sasa amerejea nchini mwake anashuhudia kuwa burundi ina amani na kuwahikiza waliosalia kambini kuepuka uvumi na waamue kurejea.

Tanzania yasema bado iko fursa ya wakimbizi wa Burundi kuingia Tanzania kwa shughuli za kiuchumi

DR Kongo Flüchtlinge
Picha: ESDRAS TSONGO/AFP via Getty Images

Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andebgenye amefurahishwa na utaratibu huo huku akisema kuwa suluhisho la ukimbizi ni kurejea nyumbani na kwamba ipo fursa ya warudi kuingia tanzania kwa shughuli za kiuchumi badala ya ukimbizi

Shirika la kuhudumia wakimbizi duniani UNHCR leo linazindua mpango maalumu wa kuwahamasisha wakimbizi wa Burundi kurejea nchini mwao. Mpango huo ukiopewa jina la njoo utoe ushuhuda, unahusisha raia wa Burundi waliokuwa wakimbizi nchini Tanzania kuja kukutana na wakimbizi makambini na kuwaelezea uhalisia wa usalama na amani nchini mwao.

soma zaidi:UN Walaani udhalilishaji wa wakimbizi wa Burundi

Katika mpango huo jumla ya warundi 10 wakiwemo vijana wanawake na wazee wameongozana na viongozi wa UNHCR Burundi, viongozi wa serikali ya Burundi na wanaungana na viongozi wa serikali ya Tanzania kutembelea kambi ya wakimbizi mchanganyiko ya Nyarugusu yenye jumla ya wakimbizi 129,870 kati yao 49533 ni raia wa Burundi, na 140 kutoka Kenya, Rwanda, Uganda, Suda, Somalia na Zimbabwe

Mwandishi. Prosper Kwigize DW Kigoma