1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN Walaani udhalilishaji wa wakimbizi wa Burundi

Angela Mdungu
14 Aprili 2021

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa mataifa wametoa wito kwa Tanzania na Burundi kuheshimu haki za wakimbizi wa Burundi baada ya ripoti kuwa wanakabiliawa na mateso wakiwa katika kambi za wakimbizi za Tanzania

https://p.dw.com/p/3s0GH
Tansania Burundis Flüchtlinge
Picha: Tchandrou Nitaga/AFP/Getty Images

Zaidi ya raia 300,000 wa Burundi waliikimbia nchi yao kutokana na mgogoro wa kisiasa wa mwaka 2015 wakati aliyekuwa rais wa nchi hiyo wakati huo Pierre Nkurunziza alipogombea urais kwa muhula wa tatu, muhula uliopingwa hali iliyosababisha vurugu. Takribani watu 1,200 walikufa katika machafuko hayo.

Karibu nusu ya wakimbizi waliotokana na vurugu hizo walipata hifadhi katika kambi za wakimbizi kwenye nchi jirani ya Tanzania. Kundi la wataalamu huru 11 wa Umoja wa mataifa walitoa kauli ya kutahadharisha  kuwa Polisi nchini Tanzania na mashirika ya upelelezi waliwakamata watu kwa nguvu na walihusika na kupotea kwa wakimbizi na watafuta hifadhi wakishirikiana na taasisi za upelelezi za Burundi.

Wataalamu hao wamesema, wakimbizi wa Burundi sasa wanaishi kwa hofu ya kutekwa ifikapo usiku wa manane ambapo hupelekwa kusikojulikana ama hurudishwa kwa nguvu Burundi. Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imekuwa ikiwashawishi wakimbizi warudi Burundi kwa madai kuwa nchi hiyo sasa ni salama. Rais wa sasa wa Burundi Evarist Ndayishimiye anayetuhumiwa na wachunguzi wa haki za binadamu wa Umoja wa mataifa kwa utawala unaokiuka haki amewataka pia wakimbizi warejee nyumbani kutoka Tanzania.

Burundi Gitega | Beerdigung des ehemaligen Präsidenten Pierre Nkurunziza: Evariste Ndayishimiye hält Ansprache
Rais wa Burundi Evarist NdayishimiyePicha: Getty Images/AFP/T. Nitanga

Jumatatu, Mkurugenzi wa huduma kwa wakimbizi katika wizara ya mambo ya ndani nchini Tanzania Sudi Mwakibasi alinukuliwa na vyombo vya habari vya ndani akisema, hakuna haja ya watu kuishi kama wakimbizi wakati nyumbani kuna amani na taifa likiwasubiri kujenga taifa.

Hofu ya usalama

Maafisa wa serikali ya Tanzania hata hivyo wamesema kambi wanamokaa wakimbizi zimekuwa zikichochea hofu ya usalama. Wataalamu hao wa umoja wa mataifa wametoa tahadhari kuwa hali katika kambi hizo ni mbaya. Wamegusia pia taarifa kuwa baadhi ya watumishi wa shirika la Ujasusi la Burundi wamekuwa wakiishi kwa kujifanya wakimbizi katika kambi hizo ili kuwafahamu watu ambao baadaye walikamatwa na vikosi vya usalama vya Tanzania.

Katika ripoti yao,wataalamu hao wa umoja wa mataifa wamesema, ni lazima Burundi iache ukandamizaji dhidi ya raia wake  wakiwemo wale wanaotafuta kulindwa kimataifa nchini Tanzania. Wamesema, hofu inayozidi kukua juu ya usalama imewafanya wakimbizi wengi ambao hawakutaka kurejea Burundi kufanya hivyo.