1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake Sudan bado walilia haki baada ya Bashir kuanguka

8 Machi 2020

Wanawake wa Sudan walikuwa msitari wa mbele katika maandamano yaliomuangusha Omar al-Bashir, lakini miezi 11 badae, wanaharakati wanalalamikia ukosefu wa hatua kuhusu masuala ya wanawake.

https://p.dw.com/p/3Z2Ru
BG Frauen im Sudan
Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Mwanaharakati aliehusika kuanzia mwanzo wa vuguvuvu la maandamano yaliohitimisha utawala wa miongo mitatu wa Omar al-Bashir, Zeineb Badreddine, ataongoza maandamano mbele ya wizara ya sheria Jumapili kuadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake. "Hakuna kilichofanyika kutekeleza madai ya wanawake," alisema Badreddine.

Karibu miaka 30 baada ya kufukuzwa kazi chini ya Bashir kutokana na "dhana zake za mageuzi na haki za kiraia", hivi sasa amerejea kwenye ufundishaji. Lakini licha ya kupinduliwa kwa utawala wa Bashir, anasema serikali mpya inakosa uwakilishi wa wanawake.

Baada ya waziri mkuu Abdalla Hamdok kuunda serikali yake mwezi septemba, aliahidi kuobresha hali ya wanawake licha ya ugumu wa kiuchumi na kijamii nchini humo. Alitoa nafasi 17 za mawaziri kwa wanawake, ikiwemo wizara nyeti ya mambo ya kigeni. Mwanamke pia aliteuliwa kuongoza idara ya mahakama.

BG Frauen im Sudan
Wanawake wa Sudan wakiwa na michora ya bendera ya taifa hilo katika nyuso zao. Wanaharakati wa haki z wanawake nchini humo wanasema masuala yao hayajshughulikiwa ipasavyo miezi 11 tangu kuondolewa kwa Omar al-Bashir.Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Lakini mamlaka ya juu kabisaa ya nchi, Baraza la uongozi linaloundwa kwa pamoja kati ya raia na jeshi likiwa na mamlaka ya kusimamia kipindi cha mpito kuelekea utawala wa kiraia, lina wawakilishi wawili tu wa kike katika ya jumla ya wajumbe 11. "Iwapo wanawake wangekuwa na uwakilishi mzuri, wangekuwa na sauti zaidi za kuwatetea," alisema Badreddine.

Sheria kandamizi dhidi ya wanawake

Chini ya utawala wa Bashir, sheria ya "utulivu wa kijamii" ilitumika kuwaadhibu wanawake hadharani au kuwafunga gerezani kwa uvaaji usiyo wa heshima au kunywa ulevi, vitendo vilivyotazamwa kama ukosefu wa heshima na maadili.

Serikali ya Hamdok iliondoa sheria hiyo mwaka jana - lakini sheria nyingine nyingi za kibaguzi zinaendelea kutumika. Badreddine analalamikia sheria ya jinai kuhusu unyanyasaji wa kingono. Majaji nchini Sudan wana mamlaka ya kuamua iwapo mwanamke amebakwa au la, jambo ambalo wakati mwingine linapelekea waathirika kushtakiwa kwa uzinzi.

Wakili na mwanaharakati wa wanawake Inaam Atiq anakosoa sheria ya hadhi binafsi ya mwaka 1991, ambayo anasema "inasababisha mateso kwa maelfu ya wanawake kote Sudan." Anasema sheria hiyo inaruhusu watoto wa kike wenye umri wa miaka 10 kuozeshwa kinyume na matakwa yao.

Asma Mohamed Abdalla Außenministerin Sudan
Waziri wa mambo ya nje wa Sudan Asma Mohamed Abdalla, moja ya wanawake walioko kwenye nafasi muhimu serikalini.Picha: AFP/E. Hamid

"Maandishi haya yanapaswa kurekebishwa haraka na hili linaweza kufanyika vila kugusa  kanuni za Sharia (Sheria ya Kiislamu)," alisema. Sheria nyingine inawapiga marufuku wanawake kusafiri nje ya nchi hadi wapate ruksa kutoka kwa msimamizi wa kiume -- hatua iliyofutwa hata na Saudi Arabia. "Msimamizi wangu anaweza kuwa mdogo wangu wa kiume niliemlea, au hata mwanangu," alisema Atiq.

Na hata mahakama zinazoshughulikia masuala ya hadhi binafsi hayazingatii matokeo ya vipimo vya vinasaba (DNA), yanayoruhu wanaume kushiriki katika malezi ya watoto, suala ambalo linazidisha masaibu ya wanawake, alisema.

Mwanaharakati Manal Abdelhalim anaeleza kushangazwa na sauti, zikiwemo za wanawake, wanaosema kwamba suala la (haki za wanawake) siyo la kipaumbele na kwamba linaweza kusubiri."

Lakini Atiq anayo matumaini.

"Tunahitaji hatua za mara moja, na nadhani wizara ya sheria and serikali zinaelewa hali," anasema. "Nina matumaini kuhusu uwezekano wa kuchukuwa hatua katika mwelekeo sahihi."

chanzo: afpe