1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake nchini Kenya wapigania haki zao zilindwe na katiba.

Mohammed Abdulrahman26 Mei 2004
https://p.dw.com/p/CHii
Rais Kibaki alipokua akiapishwa Desemba 30,2002.
Rais Kibaki alipokua akiapishwa Desemba 30,2002.Picha: AP

Nchini Kenya-wakati muda wa mwisho ukizidi kukaribia, kabla ya kukamilishwa katiba mpya, wanaharakati wanaopigania haki za wanawake nchini humo wanashauku kubwa juu ya mabadiliko yajayo chini ya zingatio la kwamba katiba ya sasa inawabagua wanawake. Zaidi kuhusu haki za wanawake katika mapendekezo ya katiba mpya ya Kenya

Pale Rais Mwai Kibaki aliposhika rasmi wadhifa huo mwishoni mwa mwezi Desemba 2002, aliahidi kwamba Kenya itakua na katiba mpya katika muda wa siku 100. Waraka huo unaangaliwa kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kuelekea katika utawala katika taifa hilo la Afrika mashariki, kushajiisha maendeleo na kuondoa umasikini. Hata hivyo mivutano ya kisiasa iliozuka baadae ikasababisha kushindwa kufikiwa muda huo na kipindi cha mwisho cha kukamilishwa katiba hiyo kuwa Juni 30 mwaka huu.

Katiba ya zamani imewageuza wanawake kuwa daraja ya pili katika jamii-anasema hayo mwanaharakati Atsango Chesoni ambaye ni mpigania haki za wanawake na mjumbe katika mazungumzo ya katiba yanayofanyika huko Boma nje ya mji mkuu Nairobi. Wanawake wengi wameathirika baada ya vifo vya waume zao au kutokana na kuachwa, kwani hubaguliwa na jamaa wa Marehemu na kukosa hata haki zao za urithi kutokana na sheria zinazotajwa ni za kijadi. Sheria ya urithi nchini Kenya huenda sambamba na desturi za kijadi na hivyo kumzuwia mwanamke kudai mali ya mumewe.

Maria Nekesa, alipoteza mali yote baada ya kuzuiliwa na jamaa za marehemu mumewe alipofariki miaka minne iliopita na kulazimika kutapia maisha upya pamoja na watoto wake wawili. Akisimulia yaliomsibu alisema alipokonywa kila kitu ikiwa ni pamoja na ardhi ya hekari sita. Hayo yalimfika baada ya ndugu zake marehemu mumewe kutaka yeye Maria pia alithiwe na mdogo wake marehemu na alipokataa akatolewa ndani ya nyumba pamoja na wanawe.

Juhudi zake kutaka msaada wa serikali ziligonga mwamba. Akalazimika kupeleka malalamiko yake kwa Chifu wa kabila lao, ambaye alimjibu kuwa hilo ni tatizo la kifamilia na anapaswa kulitatua na shemeji zake. Maria ni mfano mmoja tu, lakini wanawake wengi wamejikuta katika hali kama hiyo.

Kifungu cha 77 katika ibara ya saba ya katiba kinataja kwamba"serikali itafafanua na kuipitia upya sera ya ardhi ya taifa, ikihakikisha desturi za kijadi haziwabagui wanawake kuwa haki ya kumiliki ardhi panapohusika na urithi. Inataja kwamba mke (mjane) hawezi kunyimwa haki ya kurithi mali ya mumewe (marehemu) bila kujali kama aliandika wasia au la.Bibi Anna Njogu anasema kama kifungu hicho kingekua ni sheria kamili leo hii, basi wanawake wasingebaguliwa .

Hata hivyo mratibu wa jumuiya inayopambana na matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake, Anna Gathumbi, ana shaka shaka akisema kuwa na katiba ni kitu kimoja na utekelezaji wa yaliomo katika katiba hiyo ni kitu kingine. Akasema huenda ikawa ni vigumu kwa wanawake masikini kuwa na nguvu za kuweza kukabiliana na jamaa zao na kupinga tabia ya kuwanyima haki zao, hata kama katiba inawapa haki hiyo.

Mapendekezo mengine yaliozusha mabishano katika muundo wa katiba mpya itakayopendekezwa ni pamoja na kupunguza nguvu za madaraka ya Rais na kuyahamishia kwa waziri mkuu. Mapendekezo hayo yamezusha mabishano makali katika serikali ya muungano ya NARC ya Rais Kibaki, huku baadhi wakiamini kwamba Kiongozi huyo wa taifa anakiuka makubaliano na ahadi za hapo mapema kwamba angeunga mkono kuwepo kwa Rais asiye na madaraka makubwa ya utendaji.

Kutokana na vuta nikuvute hiyo, sasa muda wa mwisho wa kuwasilishwa mapendekezo ya katiba hiyo mpya na kutiwa saini kuwa sheria ni Juni 30. Tayari wanaharakati wanasema wataitisha maandamano ya umma ikiwa hadi tarehe hiyo, katiba hiyo haitoidhinishwa. Maandamano hayo yanaungwa mkono na Shirikisho la wanasheria wanawake nchini Kenya. Joyce Majiwa anasema"kama hakuna kitakachofanywa hadi tarehe 30 Juni basi patahitajika hatua zitakazotoa msukumo kwa wahusika kutekeleza matakwa hayo." Wanaharakati wanasema baada ya mabadiliko ya Desemba 2002, yaliopelekea kun´golewa madarakani kwa utawala wa tangu uhuru 1964 wa chama cha KANU na kuingia madarakani muungano wa NARC, wanachohitaji sasa wananchi wa Kenya ni katiba mpya .