1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanamgambo watikisa usalama Kinshasa

17 Mei 2023

Mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa unatishiwa na ukosefu wa usalama unaosababishwa na wanamgambo wa Mobondo, waliotokana na mzozo baina ya jamii za Wateke na Wayaka za jimbo la Bandundu.

https://p.dw.com/p/4RUWg
Konflikt im Kongo
Picha: Alexis Huguet/AFP

Wakati mzozo baina ya jamii za Wateke na Wayaka ukisababisha mamia ya watu kupoteza maisha na maelfu kuyahama makaazi yao katika maeneo ya Kwamouth na Bagata jimboni Bandundu lililo umbali wa kilomita 150 kutoka Kinshasa, wanamgambo wa Mobondo tayari wanatatiza manispaa ya Maluku ambako mwishoni mwa wiki iliyopita waliua watu 11. 

Serikali ya mji wa Kinshasa ilimtuma huko jana Jumanne waziri wake wa mambo ya ndani, Gratien Tsakala, ili kutathmini hali ya usalama, ambaye aliwaomba wakaazi  kuwa waangalifu.

Soma zaidi: Watu 5 wauawa kwenye shambulizi Kongo

"Wakaazi wa sehemu hii ya mji mkuu wanaishi katika hali ya ukosefu wa usalama iliyosababishwa na wanamgambo wanaoitwa Mobondo. Ilinibidi kwenda huko ili kujua hali halisi na kutoa ujumbe wa faraja kwa watu hawa na kuwaomba kuwa waangalifu. Hii pia ni fursa kwangu kuomba wakazi wa wilaya ya Maluku kuwa na imani kwa vikosi vya ulinzi wa usalama vinavyotumwa usiku na mchana ili kurejesha utulivu." Alisema waziri huyo.

Wabunge wataka kuundwa kamati maalum

Konflikt im Kongo
Wanajeshi wa Burundi wakiwasili nchini Kongo kulinda usalama.Picha: Alexis Huguet/AFP

Haya yanajiri miezi saba kabla ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Desemba 20 mwaka huu, huku bunge la mji wa Kinshasa limewasilisha swali hilo la ukosefu wa usalama kwa Spika wa Bunge la kitaifa.

Papy Mpiana, ambaye ni mbunge wa mji wa Kinshasa, anapendekeza kuundwa  tume ya taasisi mbalimbali ili kutafuta suluhu la mgogoro baina ya jamii za Wateke na Wayaka.

Soma zaidi: Mwanajeshi mmoja na wanamgambo 4 wauwawa kwenye shambulizi nchini Kongo

“Tunapendekeza kuwe na tume itakayoundwa na manaibu Waziri Mkuu wa Mambo ya Ndani na wa Ulinzi, Mawaziri wa Sheria na wa Masuala ya Jamii, pamoja na magavana wanne wa mikoa inayohusika yaani Kinshasa, Kwango, Kwilu na Maindombe,  wateule wa mikoa hiyo pia viongozi wa kiadiki wa kweli." Alisema mbunge huyo.

Mashahidi wanasema wanamgambo wa Mobondo wanawauwa wahanga wao kwa mapanga, hali inayowatisha watu na kuwafanya maelfu kukimbia makaazi yao.  

Madai ya jamii ya Wateke

Konflikt im Kongo
Wanajeshi wa Burundi wakiwasili nchini Kongo.Picha: Alexis Huguet/AFP

Wateke wanadai kuwa Mobondo ni wanamgambo wa Wayaka, jambo ambalo analikanusha Jonathan Bialusuka, ambaye ni mbunge wa kitaifa.

"Hamna kiongozi wa Wayaka anayeunga mkono wamobondo ambao hatujui hata walipo. Tusiwanyanyapae Wayaka kama jamii ya wauaji. Ni muhimu askari kufanya kazi yao huku wakilinda watu wasio na hatia. Wayaka wasichukuliwe kuwa ni Mobondo ingawa miongoni mwa Mobondo kuna Wayaka." Alisema mbunge huyo.

Soma zaidi: Upinzani Kongo wapinga kuletwa kwa wanajeshi wa SADC

Hali hii ya ukosefu wa usalama inaweza kuathiri uchaguzi wa Desemba ijayo.

Tume ya uchaguzi haikufaulu kusajili wapigakura katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa waasi wa M23 mkoani  Kivu Kaskazini, pia katika maeneo ya Kwamouth na Bagata huko  Bandundu na sehemu ya wilaya ya Maluku, mkoani Kinshasa, kutokana na machafuko.

Mwandishi: Jean Noël Ba-Mweze/DW Kinshasa
Mhariri: Daniel Gakuba