1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wanaoshukiwa kuwa wa Urusi waonekana Mali

Sylvia Mwehozi
18 Agosti 2022

Vikosi vya Ujerumani vimedai kuwaona wanajeshi kadhaa wanaoshukiwa kuwa wa Urusi katika mji wa Kaskazini mwa Mali wa Gao mapema Jumatatu, siku ambayo kundi la mwisho la wanajeshi wa Ufaransa liliondoka nchini humo.

https://p.dw.com/p/4Fj0i
Afrika Wagner group in Mali
Picha: French Army/AP/picture alliance

Kamandi ya kijeshi ya operesheni za pamoja ya Ujerumani ilisema katika barua yake iliyoonwa na shirika la habari la Reuters kwamba, siku ya Jumatatu wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kutoka Ujerumani na Uingereza waliziona ndege mbili katika uwanja wa ndege wa Gao. Barua hiyo ilikuwa imeelekezwa kwa kamati ya bunge ya ulinzi na mambo ya kigeni, na kuripotiwa kwa mara ya kwanza na jarida la Spiegel. Barua hiyo ilikwenda mbali na kusema kwamba Urusi ilikuwa imekabidhi ndege aina ya L-39 kwa vikosi vya Mali wiki iliyopita.Ufaransa na Washirika wake waamua kuondoka Mali

Taarifa hiyo iliongeza kuwa "watu 20 hadi 30 waliovalia sare za kijeshi ambazo si za Mali, walionekana wakishusha vifaa kutoka ndege ya Mali". Kulingana na barua hiyo, watu hao wanashukiwa kuwa wanajeshi wa Urusi lakini haikufahamika mara moja walikuwa na kazi gani mjini Gao.

Bundeswehr-Einsatz in Mali
Wanajeshi wa Ujerumani chini ya kikosi cha MINUSMAPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Ufaransa ilitangaza Februari kwamba inaondoa wanajeshi wake kutoka Mali, baada ya kutofautiana na utawala wa kijeshi wa nchi hiyo. Kuwasili kwa wapiganaji wa Urusi nchini Mali kunatokana na mwaliko wa serikali ilikuwa ni sababu kuu ya uamuzi wa Ufaransa wa kuondoa wanajeshi wake. Wanajeshi wa mwisho wa Ufaransa waliondoka Mali siku ya Jumatatu.Makundi ya kigaidi nchini Mali yashambulia kambi ya jeshi

Hayo yakijiri, jeshi la Ujerumani limeanza tena safari za ndege kuelekea Mali baada ya Berlin kusitisha safari zake nyingi katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi katika mzozo na mamlaka ya anga juu ya vibali vya kurusha ndege.

Berlin imetuma takriban wanajeshi 1,000 nchini Mali, wengi wao karibu na mji wa kaskazini wa Gao ambapo kazi yao kuu ni kukusanyika taarifa za kiuchunguzi kwa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa MINUSMA. Kikosi cha MINUSMA nchini Mali kilianzishwa mwaka 2013 kulisaidia taifa hilo kukabiliana na wapiganaji wa itikadi kali.

Wakati huo huo Mali imeishutumu Ufaransa kwa kukiuka sheria yake ya anga na kutoa silaha kwa wapiganaji wa Kiislamu katika jaribio la kuiyumbisha nchi hiyo ya Afrika Magharibi. Katika barua kwa mkuu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa iliyoandikwa Jumatatu, waziri wa mambo ya nje wa Mali, Abdoulaye Diop, alisema anga yake imekiukwa zaidi ya mara 50 mwaka huu, zaidi na vikosi vya Ufaransa kwa kutumia ndege zisizo na rubani,  helikopta za kijeshi pamoja na na ndege za kivita.