1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Eritrea waondoka kaskazini mwa Ethiopia

30 Desemba 2022

Nchini Ethiopia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miezi 18, polisi wameanza kuhudumu katika mji mkuu wa Tigray, Mekele na wakati huo huo wanajeshi wa Eritrea wameondoka kutoka kwenye miji ya kaskazini mwa Ethiopia.

https://p.dw.com/p/4LaE3
Eritrea Äthiopien Soldaten Flash-Galerie
Picha: AP

Hatua hiyo inaashiria kuanza kufanya kazi mkataba wa amani wa kusitisha mapigano uliotiwa saini mwezi uliopita kati ya serikali kuu ya Ethiopia na viongozi wa jimbo la Tigray umeutuliza mzozo wa miaka miwili ambao umesababisha kuuliwa maelfu ya watu na wengine mamilioni wamelazimika kuyahama makazi yao.

Idara ya polisi wa shirikisho iliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba maafisa wake katika mji wa Mekele watatimiza wajibu wa kulinda mali na usalama wa watu kwa mujibu wa katiba ya nchi ikiwemo kutoa ulinzi kwenye viwanja vya ndege, mitambo ya umeme na ya mawasiliano ya simu pamoja na benki.

Mabinti wameshikilia bango kuunga mkono mkataba wa amani uliotiwa saini kati ya serikali kuu ya Ethiopia na mamlaka ya jimbo la Tigray.
Mabinti wameshikilia bango kuunga mkono mkataba wa amani uliotiwa saini kati ya serikali kuu ya Ethiopia na mamlaka ya jimbo la Tigray.Picha: AP Photo/picture alliance

Vilevile huduma za kimsingi na misaada ya kibinadamu vimeanza tena kuingia hatua kwa hatua katika jimbo la kaskazini la Tigray. Waziri wa Afya wa Ethiopia Lia Tadesse, amesema tangu kuanza tena kupelekwa huduma za misaada, vifaa vya kuokoa maisha vya zaidi ya dola milioni nne za Marekani vimefikishwa katika jimbo la Tigray na katika msaada huo zipo chanjo na bidhaa zingine za thamani ya dola milioni mbili nukta tisa zinazohusiana.

Hatua nyinginezo ni pamoja na miji ya Adirkay, Enchiko, May Tsebri na Rama kuunganishwa tena kwenye gridi ya taifa baada ya kukatishwa kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu. Shirika la ndege la Ethiopia, limetangaza kuwa litaanza tena safari zake kuelekea katika mji wa Shire na pia litaongeza safari za ndege kuelekea katika mji mkuu wa Tigray, Mekele.

Soma:Ethiopia na TPLF kuunda chombo cha kusimamia makubaliano ya amani

Siku ya Alhamisi, wajumbe kutoka Umoja wa Afrika na wa serikali kuu ya Ethiopia walifika katika mji wa Mekele kuanzisha ujumbe utakaofuatilia maendeleo katika utekelezaji wa makubaliano hayo ya amani.

Majenerali watatu wa kiafrika wamepewa jukumu la kuongoza ujumbe huo wa wafuatiliaji na wakati huo huo mabalozi kutoka nchi 32 walikwenda mjini Mekele siku ya Alhamisi.

Huku hayo yakiendelea baadhi ya watu wameliambia shirika la Habari la Reuters kwamba wanajeshi wa Eritrea, waliopigana kuwaunga mkono wanajeshi wa serikali ya Ethiopia wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka miwili iliyopita katika mkoa wa kaskazini wa Tigray wameondoka kutoka kwenye miji ya Shire na Axum.

Äthiopien Der erste Flieger landete regionalen
Picha: Million Haileselassie/DW

Haijabainika mara moja iwapo wanajeshi hao wa Eritrea watakuwa wameondoka kabisa kutoka Tigray au ni hatua ya kusogea nyuma kutoka kwenye miji fulani tu. Waziri wa Habari wa Eritrea Yemane Gebremeskel alipozungumza na shirika la habari la Reuters hakuthibitisha wala kukanusha na pia hakufafanua juu ya zoezi hilo la kuondoka kwa askari wa Eritrea.

Kwa jumla wapatanishi wa serikali kuu ya Ethiopia na wa mamlaka katika jimbo la Tigray wanapiga hatua katika kuongeza juhudi za kuhakikisha kwamba mapatano ya amani yanatekelezwa wakati ambapo mahusiano kati ya pande hizo mbili yanaelekea kurejea katika hali ya kawaida.

Vyanzo: RTRE/AP/AFP