1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati wakemea vitendo vya ukiukwaji haki za binadamu

Saumu Mwasimba27 Januari 2006

Mkutano wa kimataifa unaojadili masuala ya kijamii huko Caracas Venezuela unaendelea.

https://p.dw.com/p/CHns
Mjini Caracas
Mjini CaracasPicha: AP

Mwanaharakati wa Haiti katika mkutano huo ameitaka jamii ya kimataifa kutoa sauti dhidi ya kile alichokitaja kuwa ni vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyoungwa mkono na Marekani nchini Humo.

Wanaharakati katika mkutano huo pia wamekosoa matatizo wanayoyapata wanawake wanaoishi katika umaskini katika mataifa ya Amerika ya Kusini.

Akizungumza kwenye mkutano huo uliongia siku yake ya tatu hii leo,wakili wa haki za binadamu nchini Haiti Mario Joseph aliishutumu Marekani kwa kuwa chanzo cha matatizo nchini Haiti.

Haiti imeharibika kutokana na machafuko na ukosefu wa usalama tangu kupinduliwa kwa rais wa zamani Jean-Bertrand Aristide chini ya hinikizo za Marekani mnamo Februari mwaka 2004.

Mario ambaye ni mwanachama wa kundi la kidemokrasi linalodhaminiwa na Aristide nchini Haiti amedai mahakimu nchini humo wako chini ya hinikizo kubwa kutoka Marekani,Canada na Ufaransa,nchi amabazo zimechangia majeshi katika vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa nchini Haiti.

Wakati huo huo wanaharakati kwenye mkutano huo wa kimataifa unaojadili masuala ya kijamii wamekosoa vikwazo wanavyokumbana navyo wanawake maskini wanaishi katika mataifa ya Amerika ya Kusini wakisema kwamba wanawake hao wamekuwa ni wahasiriwa wasiosikizwa kilio chao duniani.

Maria Goresi wa Brazil na Carlos Carlos wa Venezuella wakiwa mjini Caracas kwenye mkutano huo unaojadili masuala ya kijamii duniani walikuwa na risala ya kutoka kwa walal hoi kuwafikia wanaojiweza walioko huko Davos wanasema…..

``Iwapo Kila kitu kitanzuliwe kwa njia tu ya kiuchumi ni jambo amabalo halitawezekana.Lazima tujenge dunia yenye kumlinda mwanadamu na mahitaji yake ya kijamii.Amerika ya kusini itakua ni msingi kwani hapa tunaweza kuonesha kwamba kuna maisha ya aina nyingine ambayo yanaweza kuchipuka na tusiwe na Uoga ila ni lazima tusaidiane``

Makundi mengi ya kutetea haki za wanawake yameeleza kuwa hatua ya kuelekea masoko huru inadhoofisha msimamo wa wanawake katika eneo hilo ambako bado wanaume wanausemi mkubwa, na ambako ukatili majumbani bado ni tatizo kubwa na serikali zimechukua msimamo mkali dhidi ya utoaji mimba.

Baadhi ya wanaharakati hao wanabisha kwamba sera za soko huru zimeharibu sekta ya uchumi ya mataifa ya Amerika ya Kusini kama vile Kilimo ambacho hutoa ajira kwa idadi kubwa ya asilimia ya wanawake.

Kwa mujibu wa wanaharakati Mataifa ya Amerika ya kusini na Caribbean yamegeukia biahsara ya utalii kama njia ya kujipatia mapato na kuzusha kuongezeka kwa biashara ya ukahabaambayo inasababisha wanawake kuuzwa katika biashara hizo haramu.

Washiriki katika mkutano huu wa kimataifa pia wamewataka walinda amani wa Umoja wa Mataifa kuondoka nchini Haiti na nchi masiki zisamehewe madeni na pia wameliunga mkono pendekezo la rais Fiedel Castro wa Cuba la kutaka kuwepo mahakama maalum ya kuchunguza sera dhidi ya Ugaidi ili kuupinga ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Marekani dhidi ya nchi maskini.

Rais Hugo Chavez amewakaribisha wanaharakati hao katika mkutano akisema mawazo yanayojadiliwa katika kikao hicho yamewahamasisha watu na kusaidia katika kulipinga pendekezo linaloungwa mkono na Marekani la kuwepo kwa biashara huru.