1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanafunzi 17 wafariki kwa kuteketea moto Kenya

6 Septemba 2024

Watoto 17 wa shule ya msingi wamekufa kwa kuungua moto wakiwa bwenini, kwenye shule ya msingi ya Hillside Endarasha Academy nchini Kenya.

https://p.dw.com/p/4kLvg
Kenya Nyeri | Moto kwenye bweni | Shule ya msingi ya Hillside Endarasha
Wazazi waliofadhaika wamesimama karibu na bweni lililoteketea kwa moto katika shule ya msingi ya Hillside Endarasha mjini NyeriPicha: AP Photo/picture alliance

Taarifa ya polisi nchini Kenya imesema moto huo uliwaka usiku wa manane wakati watoto hao walipokuwa wamelala.

Msemaji wa jeshi la polisi nchini humo, Resila Onyango, amesema wanafunzi kadhaa wamejeruhiwa, 16 kati yao wakiwa na majeraha makubwa na wamepelekwa hospitali.

Ameongeza kuwa baadhi ya miili ya wanafunzi waliokufa imeungua kiasi cha kutotambuliwa. Chanzo cha moto bado hakijajulikana.

Soma pia: Mwanariadha wa Uganda afariki baada ya mpenzi kumchoma moto 

Rais William Ruto ametoa salamu za rambirambi kwa familia za wanafunzi waliokufa katika ajali hiyo.

Kupitia mtandao wa kijamii wa X, kiongozi huyo amesema anaomboleza vifo vya wanafunzi hao na kuzitaka mamlaka husika kufanya uchunguzi kamili kubaini chanzo cha moto huo na watakaopatikana na hatia kuchukuliwa hatua za kisheria.