1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliouwawa kwa risasi Hamburg wafikia 8

Angela Mdungu
10 Machi 2023

Polisi mjini Hamburg nchini Ujerumani wamesema kuwa watu wanane wameuwawa baada ya mtu mmoja kufyatua risasi kwenye nyumba ya ibada ya mashahidi wa Yehova Alhamisi jioni

https://p.dw.com/p/4OUsS
Tödliche Schüsse auf Zeugen Jehovas | Hamburg
Picha: Gregor Fischer/Getty Images

Polisi mjini Hamburg nchini Ujerumani wamesema kuwa watu wanane wameuwawa baada ya mtu mmoja kufyatua risasi kwenye nyumba ya ibada ya mashahidi wa Yehova Alhamisi jioni. Kwa mujibu wa jarida la Spiegel Magazine la nchini humo bila kutaja chanzo limeandika kuwa, mmoja wa waliouwawa ni mwanamume mwenye umri wa kati ya miaka 30 na 40 anayetuhumiwa kuwa ndiye aliyefanya tukio hilo.

Polisi mjini Hamburg wanaendelea kufanya uchunguzi wakitaka kujua chanzo cha mtu mmoja kuwafyatulia risasi wafuasi wa dhehebu la mashahidi wa Yehova. Wanapeleleza ikiwa mtu huyo alifanya mauaji hayo peke yake katika tukio. Nalo gazeti la Bild la nchini humo limeripoti kuwa watu wengine saba wamejeruhiwa katika tukio hilo.

Soma pia:Scholz alaani shambulizi la Hamburg 

Deutschland | Bundestag Bundeskanzler Scholz Regierungserklärung Zeitenwende
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz kupitia ukurasa wake wa twitter amelaani tukio hilo akikiita kitendo hicho cha mauaji kuwa ni ukatili. Ametoa pole kwa walioathiriwa na tukio hilo pamoja na familia zao akisisitiza kuwa vikosi vya usalama vinakabiliwa na operesheni ngumu. Jeshi la polisi linatarajiwa kufanya mkutano na waandishi wa habari mchana huu ili kutoa taarifa zaidi kuhusu tukio hilo. Awali Picha za Televisheni zilionesha magari kadhaa ya polisi yakifunga mitaa, magari ya huduma za dharura yakiwa na watoa huduma  huku baadhi ya watu wakiwa wamefunikwa kwa mablanketi na kuingizwa kwenye magari.

Mtu moja kati ya walioshuhudia tukio hilo ameeleza hali ilivyokuwa wakati wa mauaji hayo akisema: "Mimi ni mkaazi hapa na nilisikia milio ya risasi kisha nikaenda dirishani kupata picha kamili ya hali. Ndipo nikaona mtu akifyatua risasi, akiwa amebeba silaha na nikachukua video''

Viongozi wengine wazungumza

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Nancy Feaser amesema wapelelezi wanafanya juhudi za kufahamu hasa chanzo cha tukio hilo.  Naye meya wa  Hamburg   Peter Tschentscher kupitia ukurasa wake wa Twitter ameelezea mshtuko wake juu ya mauaji hayo. Katika kauli yao ya pamoja kwenye tovuti yao mashahidi wa Yehova wamesema jumuiya ya waumini imeathiriwa pakubwa na tukio hilo la kutisha lililotokea kwenye jengo la Kingdom Hall baada ya ibada.

Nchini Ujerumani kuna zaidi ya mashahidi wa Yehova 175,000 kati ya hao 3,800 wanaishi Hamburg. Mashahidi wa Yehova ni vuguvugu la Kikristo ambalo asili yake ni Marekani na linafahamika kwa mahubiri yake yanayosisitiza kuepuka vurugu. Wafuasi hao wa kikristo wanafahamika pia kwa njia yao ya kueneza injili nyumba kwa nyumba.