1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakaazi wa Addis Ababa watakiwa kusajili silaha zao

2 Novemba 2021

Maafisa wa mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa wamewataka wakaazi wa mji huo wasajili silaha zao katika siku mbili zijazo baada ya vikosi vya waasi kutoka kwenye jimbo la Tigray kusema vinafikiria kuingia mjini humo.

https://p.dw.com/p/42StW
Äthiopien Mekele | Pro-TPLF Rebellen
Picha: YASUYOSHI CHIBA/AFP

Vyombo vya habari vya serikali vimetangaza Jumanne kuwa wito huo umetolewa baada ya chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF kusema kuwa vikosi vyake vimechukua udhibiti wa miji miwili ya Dessie na Kombulcha katika jimbo jirani la Amhara.

Taarifa hiyo pia imesema watu wanaosababisha vurugu wamekamatwa, bila kutoa ufafanuzi zaidi. Msemaji wa serikali ya shirikisho, Legesse Tulu hakupatikana mara moja kuzungumzia suala hilo.

TPLF yaungana na Oromo

Jumatatu usiku, vikosi vya Tigray vilisema vimeungana na wapiganaji kutoka kabila la Oromo ambao pia wanapambana na serikali ya shirikisho na vimesema vilikuwa vinafikiria kuingia mjini Addis Ababa. Oromo ni kabila kubwa la Ethiopia na viongozi wake wengi wa kisiasa kwa sasa wamefungwa gerezani.

Soma zaidi: Vikosi vya Tigray na Oromo vyaiteka miji Ethiopia

Huku hayo yakijiri Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed amewataka raia wa nchi hiyo kuongeza juhudi za kukabiliana na vikosi vya Tigray, huku kukiwa na wimbi jipya la kuwakamata watu wa kabila la Tigrinya. Mwandishi habari wa shirika la habari la Ujerumani, DPA amethibitisha kuyaona magari mawili yaliyowabeba Watigrinya ambao wengine walikuwa wakipiga kelele wakiuliza wamefanya kitu gani na kwamba hawana hatia.

Äthiopien | Premierminister Abiy Ahmed Ali
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy AhmedPicha: Office of the Prime Minister Ethiopia/UPI Photo/Newscom/picture alliance

Operesheni hiyo ya kukamata watu inatokana na mapigano yanayoongezeka ambapo wanajeshi wa Tigray wamepiga hatua kuelekea upande wa kusini. Abiy pia amevikosoa vikosi vya kigeni ambavyo hajavitaja kwa kuwaunga mkono wapiganaji wa TPLF. Amesema vikosi vya kigeni vimeongezeka kwa kasi katika mapigano na amevitaka vikosi vya serikali kupambana navyo.

Uchunguzi kuwekwa hadharani

Wakati huo huo, uchunguzi wa shirika pekee la kutetea haki za binadamu ambalo limeruhusiwa kuingia Tigray utachapishwa Jumatano, mwaka mmoja baada ya vita kuanza. Hata hivyo, watu wanaofuatilia uchunguzi huo wamesema umedhibitiwa na maafisa ambao hivi karibuni walimfukuza afisa wa Umoja wa Mataifa aliyekuwa akisaidia kuongoza uchunguzi huo.

Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binaadamu kama vile Human Rights Watch na Amnesty International pamoja na vyombo vya habari vya kigeni bado yamezuiwa kuingia kwenye jimbo la Tigray. Hivyo ripoti hiyo inaweza kuwa chanzo pekee rasmi cha habari ulimwenguni kuhusu ukatili uliofanywa katika vita hivyo vilivyoanza Novemba mwaka 2020.

Uchunguzi wa pamoja wa ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa na Tume ya kutetea Haki za Binaadamu ya Ethiopia, EHRC iliyoanzishwa na serikali, ni ushirikiano usio wa kawaida ambao ulizusha wasiwasi miongoni mwa watu wa kabila la Tigrinya, mashirika ya haki za binaadamu na waangalizi wengine kuhusu suala la kutokuwepo upendeleo na ushawishi wa serikali.

(AP, DPA, Reuters)