1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya waasi wa Tigray na Oromo vyateka miji Ethiopia

1 Novemba 2021

Makundi mawili tofauti yanayopambana dhidi ya serikali kuu ya Ethiopia yanasema yameteka miji siku ya Jumapili, huku waziri mkuu Abiy Ahmed akiwatolea wito raia kujiunga na mapambano, katika mzozo unaozidi kuchacha.

https://p.dw.com/p/42Pwq
Äthiopien Mekele | Pro-TPLF Rebellen
Picha: YASUYOSHI CHIBA/AFP

Waasi wa Tigray wametangaza Jumapili kuuteka mji wa kimkakati kaskazini mwa Ethiopia, lakini serikali ilikanusha madai hayo, na kusema vikosi vya shirikisho vilikuwa katika mapigano makali ya kuutetea mji huo wa Kombolcha na mji mwingine wa Dessie.

Iwapo itathibitishwa, kutekwa kwa Kombolcha Jumapii, kunakojiri siku moja baada ya waasi kudai kuudhibiti mji wa Dessie, itakuwa mafanikio ya kimkakati kwa wapiganaji wa Tigray  dhidi ya jeshi la Ethiopia na washirika wake, wanaojaribu kuwafurusha Watigray kutoka mkoa wa Amhara.

Msemaji wa chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray TPLF, Getachew Reda, alisema kupitia ukurasa wa twitter kuwa wapiganaji wake wameiteka Kombolcha na uwanja wake wa ndege.

Soma pia:Shinikizo laongezeka dhidi ya serikali ya Ethiopia kuhusu jimbo la Tigray 

Mji huo mkubwa uko umbali wa takribani kilomita 380 kutoka mji mkuu Addis Ababa, na ndiyo mbali zaidi kusini mwa Amhara, ambako TPLF imefika tangu kuanza kuingia mkoani humo mnamo mwezi Julai. Hiyo inaashiria kwamba TPLF inaelekea karibu zaidi na mji mkuu wa Ethiopia.

Äthiopien | Straßenszene in Dessie
Mji wa Dessie unaodaiwa kutekwa na waasi wa TPLF.Picha: Tiksa Negeri/REUTERS

Wito kwa raia kujiunga na mapambano

Waziri Mkuu Abiy Ahmed amewahimiza raia kujiunga na mapigano dhidi ya TPLF baada ya vikosi hivyo vya Tigray kusema vimeichukuwa Kombolcha, ambao uko kwenye barabara kuu inayounganisha mji mkuu wa taifa hilo lisilo na njia ya bahari, na bandari ya Djibouti.

Waziri Mkuu Abiy alisema katika ujumbe wa twitter: "Watu wetu wanapaswa kujiunga na mapambano...kwa kutumia silaha yoyote na rasilimali walizo nazo kulinda, kuwafurusha na kuwazika magaidi."

Soma pia: Umoja wa Mataifa: Mzozo wa kibinaadamu unanukia Ethiopia

Mashuhuda walisema mapigano mapya yalikuwa yanaendelea pia katika mji muhimu wa Dessie, ambapo wanajeshi wa Ethiopia walikuwa wakiwaamuru wakaazi kubakia majumbani, licha ya kuripotiwa kurudi nyuma siku moja kabla.

Äthiopien l Premierminister Ahmed Abiy
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed.Picha: Amanuel Sileshi/AFP

Gatachew alisema wapiganaji wa TPLF waliichukuwa Dessie siku ya Jumamosi. Msemaji wa serikali Legesse Tulu, alikanusha madai kwamba TPLF iliiteka miji hiyo miwili, akisema wanajeshi walikuwa bado wanapambana kuchukuwa udhibiti.

Mawasiliano katika sehemu kubwa ya Ethiopia Kaskazini yamezimwa na waandishi habari wanadhibitiwa, hali inayofanya uhakiki wa madai ya uwanja wa vita kuwa mgumu.

Soma pia: Uturuki kuwa mpatanishi kati ya Ethiopia na Sudan

Kwingineko mkoani Amhara, waasi kutoka mkoa mkubwa zaidi nchini humo wa Oromia, ambao wanashirikiana na TPLF, walitangaza pia kupata mafanikio ya kimaeneo dhidi ya vikosi vya serikali.

Wakati huo huo, jeshi la Ethiopia limefanya mashambulizi ya anga dhidi ya Tigray siku ya Jumapili, ya karibuni zaidi katika kampeni ya mashambulizi iliyoanza karibu wiki mbili zilizopita, wakati jeshi hilo likiongeza matumizi ya nguvu yake ya angani.

Chanzo: Mashirika