1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Wagner Group yamtaka Zelensky atangaze kuipoteza Bakhmut

3 Machi 2023

Mkuu wa kampuni ya masuala ya kijeshi nchini Urusi, Wagner Group, amesema wapiganaji wake wameuzunguka mji wa Bakhmut mashariki mwa Ukraine, ambao Urusi imekuwa ikijaribu kuutwaa kwa miezi kadhaa sasa.

https://p.dw.com/p/4OD3K
Russland Sankt Petersburg 2022 | PMC Wagner Centre
Picha: Igor Russak/REUTERS

Kufikia asubuhi ya Ijumaa (Machi 3), Yevgeny Prigozhin alisema sehemu pekee ambayo haikuwa imechukuliwa na wapiganaji wa kundi lake "ni barabara moja kuelekea mji huo" wenye utajiri wa migodi ya chumvi na viwanda vya mvinyo. 

Mkuu huyo wa Wagner Group alimtolea wito Rais Volodymyr Zelensky kuwaamuru wanajeshi wake kuondoka kwenye mji huo.

"Ikiwa pale mwanzo tulikuwa tunapigana na jeshi lenye utaalamu, sasa tunazidi kukutana na wazee na watoto. Wanapigana lakini maisha yao mjini Bakhmout ni mafupi, labda siku moja ama mbili, wape fursa ya kuondoka kwenye mji huo." Alisema Prigozhin, ambaye ana mahusiano makubwa na Ikulu ya Kremlin, kupitia ujumbe kwa njia ya vidio.

Soma zaidi: Kansela Scholz awasili Marekani

Kwenye mkanda huo wa vidio aliwaonesha vijana wawili na mzee mmoja wakimuomba Zelensky awaruhusu kuondoka.

Kazi ngumu kwa Ukraine

Ukraine-Krieg - Soledar
Vikosi vya Ukraine vikijaribu kuulinda mji wa Barkhmut.Picha: AP/Libkos

Ukraine ilikuwa imeapa kuilinda "ngome ya Bakhmut" lakini imekuwa ikikumbana na nguvu kubwa ya jeshi la Urusi lililodhamiria kuutwaa mji huo, ambao ingawa kwao hauna umuhimu wa kijeshi lakini ni alama ya nguvu zao.

Maafisa wa Ukraine wamekiri kuwa mapigano yamekuwa magumu sana baada ya Urusi kutwaa vijiji vinavyouzunguka mji huo kwa wiki kadhaa sasa.

Hata hivyo, kwa sasa ni kiasi cha watu 4,500 tu waliosalia kwenye mji huo ulioharibiwa, ambao kabla ya vita kuanza ulikuwa na wakaazi wapatao 70,000, kwa mujibu wa maafisa wa Ukraine.

Lavrov, Blinken warushiana shutuma

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, alisema nchi yake haitayaruhusu tena mataifa ya Magharibi kuripuwa mabomba yake ya gesi na wala kamwe haitayategemea mataifa hayo kuwa washirika wake kwenye masuala ya nishati.

G20 Gipfel Indien
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov.Picha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Moscow inaamini kwamba mataifa ya Magharibi yanahusika na mripuko ulioharibu mabomba ya mafuta ya Nord Stream mnamo mwezi Septemba na inataka uchunguzi huru wa kimataifa ufanyike.

Soma zaidi: Blinken uso kwa uso na Lavrov pembezoni mwa mkutano wa G20

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken, amesema Urusi haiwezi kuachiwa kuendesha vita haramu bila ya kuchukuliwa hatua. 

Blinken amewaambia mawaziri wenzake kutoka India, Japan, na Australia wakiwa kwenye mkutano wa kile kiitwacho kundi la Quad hivi leo mjini New Delhi, kwamba ikiwa "Urusi itaachiwa kuendelea na inachokifanya Ukraine, ujumbe utakaokuwa unatolewa ni kuwa wavamizi wanaweza kufanya chochote, popote, bila hatua yoyote dhidi yao kuchukuliwa."

Blinken na Lavrov walikutana kwa mara ya kwanza hapo jana, wakihudhuria mkutano wa mawaziri wa kigeni wa mataifa ishirini yaliyo mbele kiuchumi duniani.