1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafuasi wa Trump waandamana wakidai udanganyifu wa uchaguzi

Yusra Buwayhid
15 Novemba 2020

Maelfu ya wafuasi wa Donald Trump wameandama Washington kumuunga mkono kiongozi huyo anayemaliza muda wake. Maafisa wa Marekani wametupilia mbali madai ya Trump ya kutokea udanganyifu katika uchaguzi wa Novemba 3.

https://p.dw.com/p/3lJJE
USA I Protest von Trump Unterstützern
Picha: Hannah McKay/REUTERS

 Maelfu ya wafuasi wa Rais Donald Trump wameandamana Jumamosi mjini Washington, Marekani, huku wakiimba nyimbo za kudai kiongozi huyo anafaa kuendelea kubakia madarakani kwa miaka mengine minne.

Trump na wafuasi wake wanadai kwamba kulifanyika udanganyifu kwenye uchaguzi wa Novemba 3, uliopelekea rais huyo kushindwa na Rais mteule Joe Biden, na kulazimika kuondoka Ikulu baada ya muhula mmoja tu madarakani.

Soma zaidi: Maafisa wa juu Marekani wasema uchaguzi ulikuwa salaama

Trump binafsi na msafara wake wa magari alipita katikakati ya maandamano hayo akiwa njiani akielekea kwenda kucheza gofu, huku wafuasi wake wakimshangilia naye akiwaonyesha tabasamu.

Watu wasiopungua 10,000, ambao wachache walikuwa wamevaa barakoa, walikutana katika ukumbi wa Freedom Plaza kabla ya kuandamana hadi katika mahakama kuu huku wakipeperusha bendera za kumuunga mkono Trump.

"Tulitaka kumuonyesha kuwa tunamuunga mkono, tunahisi wanajaribu kuiba uchaguzi," amesema Pam Ross, akimaanisha wapinzani wa kisiasa wa rais Trump, ambaye aliendesha gari kwa masaa nane kutoka Ohio kuja kushiriki maandamano hayo.

Kiongozi huyo wa Republican anashikilia madai yake kwamba kulifanyika udanganyifu na kwamba alimshinda Biden katika uchaguzi wa Novemba 3.

Baadae Jumamosi Trump aliandika ujumbe kadhaa katika mtandao wa kijamii wa Twitter, zenye madai kwamba mashine za kuhesabia kura zilikuwa zimedukuliwa na kwamba vyombo vya habari vilikuwa na hitilafu katika jinsi vilivyotangaza taarifa za uchaguzi huo.

Twitter kwa upande wake zimemkosoa Trump katika jumbe zake zipatazo nane, na kuchapisha onyo kwamba madai hayo siyo ya kweli.

Washington | Präsident Trump verlässt Weißes Haus | PK Impfstrategie
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: MANDEL NGAN/AFP

"Rais Trump anastahili kuungwa mkono, na anastahili kuonyeshwa upendo," Kris Napolitana, kutoka Baltimore, ameliambia shirika la habari la AFP. "Ninaamini kwamba atashinda pale udanganyifu wote na ulaghai utapofichuliwa."

Biden kutangaza baraza la mawaziri

Miongoni mwa waliohudhuria maandamano hayo, ni kundi la wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia la Proud Boys. Kutokana na hilo, usalama umeimarishwa ili kuzuia kutokea machafuko na wapinzani wa Trump nje ya Mahakama Kuu.

Makundi ya watu wanaompinga Trump walikuwa wamesimama mbali kidogo na mkusanyiko huo, huku wengine wakipiga mayoe dhidi ya wafuasi wa Trump waliokosa kuvaa barakoa.

Usiku ulipoingia, polisi waliunda mistari kila upande wa barabara inayoelekea Ikulu, wakiwatenganisha mamia ya waandamanaji wanaompinga Trump.

"Tunazuia tu watu ambao wanataka kupigana," afisa mmoja aliiambia shirika la habari la AFP.

Mapema mchana, watu wasiopungua 10 wameripotiwa kukamatwa na polisi, wanne kati yao kwa kosa la kukiuka sheria za kubeba silaha na mmoja kwa kumshambulia afisa wa polisi.

Soma zaidi: Biden aendelea na mipango ya kuunda serikali

Kura ambazo zimehesabiwa hadi hivi sasa zinampa Biden ushindi wa dahiri, akiwa amepata kura za wajumbe maalum 306 dhidi ya Trump mwenye kura 232. Kura mia mbili na sabini zinahitajika kumpa mgombea ushindi katika uchaguzi wa rais wa Marekani.

Biden Jumamosi alionekana akiendesha baiskeli katika bustani ya jimbo la Delaware na mkewe Jill wakiwa chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa usalama. Alipoulizwa ikiwa yuko tayari kuchagua baraza lake la mawaziri, alijibu "ndio."

Vyanzo: afp,ap

Mwandishi: Yusra Buwayhid

Mhariri: Babu Abdalla