1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafadhili waichangia Lebanon Euro mil. 250

10 Agosti 2020

Viongozi wa ulimwengu wameahidi kuichangia Lebanon zaidi ya Euro milioni 250 baada ya nchi hiyo kukumbwa na milipuko miwili mikubwa kwenye bandari ya mji wa Beirut.

https://p.dw.com/p/3gj0X
Frankreich Fort de Bregancon | Emmanuel Macron während virtueller Libanon-Geber-Konferenz
Picha: picture-alliance/AP Photo/C. Simon

Viongozi hao wa dunia na mashirika ya kimataifa wametoa ahadi hiyo kwa ajili ya kuisaidiia Lebanon baada ya nchi hiyo kukumbwa na maafa yaliyosababishwa na mlipuko mkubwa.

Hata hivyo viongozi na mashirika  hayo yameeleza kwamba fedha hizo zinazokusudiwa kwa ajili ya ujenzi mpya wa mji mkuu wa nchi hiyo Beirut hazitatolewa mpaka viongozi wa Lebanon watakapohakikisha kwamba watafanya mageuzi ya kisiasa na kiuchumi ambayo wananchi wanayataka.

Viongozi walioshiriki kwenye mkutano wa hapo jana walikuwa ni pamoja na rais wa Marekani Donald Trump, Mfalme Abdullah wa pili wa Jordan, rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri, viongozi wa Umoja wa Ulaya na wajumbe kutoka China. Mkutano huo uliongozwa na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.

Libanon Proteste in Beirut
Mwandamanaji akipeperusha bendera ya taifa mbele ya polisi wa kuzuwia vurugu wakati wa maandamano mjini Beirut, Agosti 8, 2020.Picha: Reuters/G. Tomasevic

Washiriki zaidi ya 30 kwenye mkutano huo wa kimataifa waliahidi msaada kwa ajili ya kufanyika uchunguzi wa kuaminika. Akizungmzia juu ya msaada kwa Lebanon, rais Donald Trump alisema:

"Kwa kuzingatia msingi wa kibinadamu tunapaswa kusaidia. Vipi nchi inaweza kuhimili maafa kama haya. Na kwa hivyo tutawasaidia kwa kiwango kikubwa.Tayari  ndege zetu kubwa tatu zimepeleka mahitaji ya dawa. Hali ni mbaya sana lakini tutawasaidia."

Soma pia: Adui mkubwa wa Lebanon ni serikali yake.

Watu nchini Lebanon kwenyewe wanataka uchunguzi ufanyike juu ya mlipuko uliotokea wiki iliyopita uliosababisha vifo vya watu wapatao 160. Watu wengine zaidi ya 6000 walijeruhiwa kutokana na mlipuko huo.

Mawaziri, wabunge wajiuzulu

Wakati huo huo mawaziri kadhaa wamejiuzulu ikiwa ni ishara jinsi serikali ya Lebanon inavyosambaratika. Waziri wa mazingira Demanios Kattar ambaye pia amejizulu amesema serikali ya Lebanon imekwama. Amesema serikali hiyo haina uwezo wa kufanya chochote.

Libanon | Information ministerin - Manal Abdel Samad
Waziri wa mawasiliano wa Lebanon Manal Abdel Samad alikuwa waziri wa kwanza kujiuzulu akisema kuna haja ya mabadiliko.Picha: Getty Images/AFP

Nchini Lebanon ikiwa idadi ya mawaziri wanaojizulu itafikia saba kati ya 20, baraza la mawaziri litalazimika kujiuzulu na nafasi yake itachukuliwa na serikali ya mpito.

Katika kadhia nyingine maandamano yameendeela kwenye mitaa ya mjini Beirut ya watu wanaotaka mageuzi. Mamia ya watu wanawalaumu viongozi wa serikali kwa usimamizi mbovu na kwa ufisadi.

Wakati huo huo Iran imesema maafa ya Lebanon hayapaswi kugeuzwa mtaji wa kisiasa na imeitaka Marekani iondoe vikwazo ilivyoweka dhidi ya Lebanon ikiwa nchi hiyo inayo dhamira ya kweli ya kuisaidia Lebanon.

Chanzo:AFP/AP/RTRE