1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafadhili waahidi dola bilioni 2.7 kwa eneo la ziwa Chad

4 Septemba 2018

Wafadhili kwenye mkutano wa kimataifa wa ngazi ya juu kuhusu mgogoro wa kibinadamu katika nchi za eneo la ziwa Chad unaoendelea mjini Berlin wanajadili namna ya kuzisaidia nchi za Afrika ya Kati.

https://p.dw.com/p/34Fe8
Berlin - Konferenz zur humanitären Krise in der Region Tschadsee
Picha: DW/A. S. Muhammad

Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imefahamisha kwamba wafadhili kwenye mkutano huo kwa pamoja wameahidi kutoa dola bilioni 2.7 za msaada kwa nchi hizo. Benki za maendeleo pia zimeahidi kutoa mikopo ya masharti nafuu jumla ya dola milioni 467.  Washiriki kutoka nchi zaidi ya 50, mashirika ya kimataifa na ya kiraia leo wanaendelea na mkutano wao mjini Berlin kujadili njia za kuleta utulivu katika eneo la Afrika ya Kati. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa watu karibu milioni 2.4 wanazikimbia nchi zao kutokana na ugaidi, umasikini na mabadiliko ya tabia nchi.

Mkutano huo wa ngazi ya juu kuhusu eneo la nchi zilizo kwenye ziwa Chad, umeandaliwa na Ujerumani pamoja na Norway, Nigeria na Umoja wa Mataifa. Mkutano huo unafanyika takriban mwaka moja na nusu tangu ulipofanyika mkutano kama huo wa wafadhili mjini Oslo nchini Norway ambao ulifanikisha kupatikana zaidi ya dola milioni 672 za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya eneo hilo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas alisema wakati wa kuufungua mkutano huo kwamba michango muhimu ya wafadhili ya mwaka uliotangulia wa 2017  iliwezesha kuzuia baa la njaa katika eneo hilo na pia kuwasaidia watu walioathirika na migogoro. Wakati huo huo waziri Maas amebainisha kwamba jitihada zaidi zinahitajika kuchukuliwa ili kuhakikisha eneo hilo halitumbukii tena katika mgogoro mkubwa zaidi.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko MaasPicha: Getty Images/AFP/Jung Yeon-je

Waziri Maas pia amewahakikishia washiriki zaidi ya 50 katika mkutano huo kutoka nchi za eneo la ziwa Chad kwamba Ujerumani inaziunga mkono nchi hizo kikamilifu. Amesema ni muhimu mkutano wa Berlin utoe ishara ya wazi kwamba washirika wote kwa pamoja  watahakikisha kuwa eneo la ziwa Chad halitakuwa kitovu cha ugaidi, uhalifu na usafirishaji wa binadamu.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema nchi yake iko tayari kuwekeza katika usalama na utulivu wa eneo hilo. Ameahidi kiasi cha Euro milioni 100 zaidi kama msaada wa nchi za kanda ya ziwa Chad.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la maendeleo la Umoja wa mataifa UNDP Achim Steiner ameiambia DW kwamba maendeleo ni suala la sera ya usalama na kutoa wito wa kutolewa msaada wa muda mrefu ili kusaidia katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Mkuu huyo wa shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP bwana Steiner amesema kwa mara nyingine jamii ya kimataifa, nchi za eneo la ziwa Chad na Umoja wa Mataifa zinazingatia kwa pamoja jinsi ya kushughulikia mpango huo mpya. Ametahadharisha kwamba iwapo misaada ya kifedha haitapatikana kwa haraka basi maana yake ni kwamba shirika hilo litasimaisha huduma zake  na hivyo kuwaacha watu katika hali ngumu mno. Mkutano huo wa siku mbili unamalizika leo hii.

Mwandishi: Zainab Aziz/Daniel Pelz/ LINK: http://www.dw.com/a-45334440

Mhariri: Iddi Ssessanga