1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Wabunge wa upinzani Uganda wafungwa jela kabla ya maandamano

23 Julai 2024

Wanasiasa watatu wa Uganda walikamatwa na kuwekwa rumande jana katika mkesha wa maandamano yaliyopigwa marufuku na serikali ya kupinga ufisadi.

https://p.dw.com/p/4ic39
Polisi wakishika doria nje ya ofisi za chama cha upinzani Uganda cha NUP
Waganda wanapanga kuandamana mjini Kampala kupinga ufisadi serikaliniPicha: SUMY SADURNI/AFP

Hatua hiyo ilijiri siku mbili baada ya Rais Yoweri Museveni, ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa karibu miongo minne, kuonya kuwa Waganda wanaopanga kuandamana mitaani leo wanacheza na moto. Msemaji wa polisi ya Uganda Kituuma Ruspke amesema wabunge hao watatu na watu wengine saba walifikishwa mahakamani jana, na kushitakiwa kwa makosa mbalimbali kuwekwa jela.

Soma pia: Upinzani wakaidi marufuku kufanya mikutano ya kisiasa kutoka kwa polisi

Hakutoa maelezo zaidi kuhusu mashitaka yao lakini msemaji wa NUP Joel Ssenyonyi alisema wabunge hao walishitakiwa kwa kukiuka sheria za barabarani na kuwazuia maafisa wa polisi, mashitaka ambayo wanayakanusha. Wabunge hao ni Francis Zaake, Charles Tebandeke na Hassan Kirumira, wote wa chama cha upinzani cha National Unity Platform - NUP na watafikishwa mahakamani Alhamisi kwa ajili ya kusikilizwa shauri lao la kuwachiwa kwa dhamana.

Hayo yanajiri wakati waandamanaji wakiapa kuendelea na maandamano yao ya kupinga ufisadi, wakihimizwa na maandamano ya kuipinga serikali yanayotarajiwa kuendelea leo katika nchi jirani Kenya. Kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine alisema kuwa vikosi vya usalama viliyazingira makao makuu ya chamachake Jumatatu.