1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Senegal: Wabunge wajadili pendekezo la kuahirisha uchaguzi

5 Februari 2024

Wabunge nchini Senegal wameanza kujadili pendekezo lililowasilishwa la kuuakhirisha uchaguzi wa rais uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe 25 mwezi huu wa Februari.

https://p.dw.com/p/4c4EH
Senegal Dakar
Polisi wakilinda doria njia ya kuingia bunge SenegalPicha: JOHN WESSELS/AFP

Wabunge nchini Senegal wameanza kujadili pendekezo lililowasilishwa la kuuakhirisha uchaguzi wa rais uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe 25 mwezi huu wa Februari.

Bunge linatathmini waraka wa pendekezo ulioidhinishwa jana na kamati ya maandalizi ,linalotaka uchaguzi uakhirishwe kwa miezi sita au hata mwaka mmoja na kufanyika Februari mwaka 2025.

Pendekezo hilo liliwasilishwa na wafuasi wa Karim Wade ambaye jina lake liliondolewa kwenye orodha ya wagombea urais na baraza la katiba la Senegal.

Soma: Watu waandamana Senegal kupinga uamuzi wa Rais kuahirisha uchaguzi

Pendekezo hilo linasema kwamba kuakhirisha uchaguzi itakuwa hatua itakayoepusha ukosefu wa uthabiti kwenye taasisi na machafuko ya kisiasa lakini pia kuhakikisha kuandaliwa kikamilifu kwa mchakato wa uchaguzi.Pendekezo hilo limeshaungwa mkono na kambi ya rais Macky Sall bungeni.

Upande mwingine ripoti zimeeleza kwamba  serikali mjini Dakar imefunga mtandao wa  mawasiliano ya simu za mkononi,huku viongozi wa upinzani na wafuasi wao wakiandamana kupinga hatua ya kuakhirisha uchaguzi.