1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji watatu wauawa katika maandamano ya Sudan

Sylvia Mwehozi
25 Januari 2022

Watu watatu wameuawa nchini Sudan, wakati maelfu ya raia kwa mara nyingine walipoingia katika mitaa ya Khartoum na katika miji mingine katika maandamano yanayoendelea tangu mapinduzi ya kijeshi miezi mitatu iliyopita

https://p.dw.com/p/463Fd
Sudan Sicherheitskräfte in Khartum
Picha: El Tayeb Siddig/REUTERS

Idadi hiyo inafanya vifo vya waandamanaji kufikia 76 tangu jeshi lilipotwaa madaraka mnamo October 25. Ukandamizaji huo mpya una uwezekano mkubwa wa kukwamisha jitihada za Umoja wa Mataifa za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa taifa hilo. Kulingana na taarifa ya Tume ya madaktari, zaidi ya waandamanaji 2,000 wamejeruhiwa tangu kuzuka kwa vurugu hizo.  Waandamanaji wengi wakiwa vijana, walimiminika katika mitaa ya Khartoum na mji pacha wa Omdurman siku ya Jumatatu, kulingana na vuguvugu la kudai demokrasia.

Maandamano kama hayo pia yalifanyika katika majimbo ya Kassala, Red Sea, Jazira na katika mkoa wa Darfur. Wanaharakati wanasema vikosi vya usalama vilifyatua risasi za moto na mabomu ya kutowa machozi ili kutawanya umati wa waandamanaji katika maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Khartoum, ikiwemo eneo lenye ulinzi mkali la ikulu ya rais. Maandamano ya mjini Omdurman pia yaligeuka kuwa ya vurugu kulingana na vuguvugu hilo. Mmoja wa waandamanaji ameapa kuendelea na maandamano.

"Tunaandamana kukataa na kulaani mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea October 25. Tuliandamana mara kadhaa na tutaendelea kuandamana, kupinga haya mapinduzi na kila kitu kilichojitokeza kutokana na mapinduzi. Tutaendelea kupambana ili tuwe na utawala wa demokrasia kwa kutumia njia za kawaida za amani."

Sudan Khartum | Protest gegen die Machtübernahme durch das Militär
Waandamanaji wanatumia tofari kuzuia mtaa mjini KhartoumPicha: Ashraf Shazly/AFP/Getty Images

Picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamiii zilionyesha maafisa wa usalama wakijaribu kuwatawanya waandamanaji kwa kutumia mabomu ya machozi. Waandamanaji nao walionekana wakijaribu kujinusuru na kuwarushia mawe maafisa wa usalama. Tume ya Madaktari wa Sudan imesema kwamba vikosi vya usalama vimewaua waandamanaji wawili mjini Khartoum, mmoja alipigwa risasi kifuani na mwingine kichwani. Mwandamanaji wa tatu alipigwa risasi begani na kichwani katika mji wa Madani kwenye jimbo la Jazira, kilometa karibu 135 kusini kwa Khartoum.

Baraza huru ambalo ni mamlaka ya juu ya Sudan linaloongozwa na jeshi, lilipokea taarifa ya kamati inayochunguza vifo vya waandamanaji na kusema katika taarifa yake kwamba, viongozi wa jeshi la Sudan wanasema kuwa haki ya maandamano ya amani bado inalindwa. Ghasia nchini humo zimeongezeka baina ya makundi yanayodai demokrasia na utawala wa kijeshi. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, umekuwa ukifanya mazungumzo na pande hasimu nchini humo katika juhudi za kupunguza msuguano baina ya viongozi wa kijeshi na vuguvugu linalodai demokrasia.