1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji 7 wauawa na vikosi vya usalama Sudan

18 Januari 2022

Vikosi vya usalama Sudan vimewauawa waandamanaji saba baada ya kuwafyatulia risasi waandamanaji Jumatatu katika moja ya mauaji mabaya kabisa kutokea hivi karibuni dhidi ya maandamano ya kupinga mapinduzi ya kijeshi.

https://p.dw.com/p/45g3D
Sudan | Proteste in Khartoum
Picha: AFP/Getty Images

Ghasia za Jumatatu, ambazo zimetokea kwenye mji mkuu wa Sudan, Khartoum na kwenye miji mingine mikubwa, zimefanyika kabla ya ziara ya wanadiplomasia wa Marekani, wakati ambapo Marekani inajaribu kusaidia kuumaliza mzozo uliodumu kwa miezi kadhaa kwenye taifa hilo la Afrika Kaskazini.

Umoja wa Mataifa walaani mauaji

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa, Volker Perthes amelaani kile alichokiita ''matumizi ya risasi za moto kwa lengo la kuzuia maandamano'', akithibitisha kuwa takriban watu saba wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa, huku ubalozi wa Marekani mjini Khartoum ukikosoa mbinu za kuzuia ghasia zinazotumiwa na vikosi vya usalama vya Sudan.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitaka serikali ya Sudan kujizuia kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji. Wanachama tisa wa baraza hilo, ikiwemo Uingereza na Ufaransa wametoa wito huo, wakisisitiza kuhusu umuhimu wa kukusanyika kwa amani na uhuru wa kujieleza.

USA New York | UN Hauptquartier - Voler Perthes zu Sudan
Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa, Volker Perthes Picha: Loey Felipe/Xinhua/picture alliance

Vifo saba vilivyotokea jana Jumatatu vinaifanya idadi ya watu waliouawa katika maandamano kufikia 71 tangu jeshi lilipofanya mapinduzi Oktoba 25 yaliyoongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.

Jumatatu, madaktari wanaopinga mapinduzi na kutetea demokrasia wamesema waandamanaji watatu waliuawa kwa kupigwa risasi na wapiganaji wa baraza la kijeshi, na baadae Kamati Kuu Huru ya Madaktari wa Sudan iliripoti kuhusu watu wengine wanne waliouawa wakati wa mauaji hayo yaliyotekelezwa na maafisa waliofanya mapinduzi.

Mmoja wa waandamanaji Hamed al-Ser amesema wanaandamana kupinga udhalimu, udikteta na utawala wowote unaokwenda kinyume na uhuru wa watu au haki yao.

"Niko hapa leo kwa sababu ninapinga mapinduzi ya kijeshi. Tuna matumaini harakati zetu zitafanikisha kuwepo utawala wa kiraia unaozingatia kidemokrasia na hatimaye watu wa Sudan watafikia malengo yao yote," alisisitiza Hamed.

Sudan Proteste
Waandamanaji wakiwa kwenye mji mkuu, KhartoumPicha: AFP/Getty Images

Wakati huo huo, Marekani imewapeleka wawakilishi mjini Khartoum katika juhudi za kuvitaka vikosi vya usalama vya Sudan kusitisha ghasia na kuheshimu haki za waandamanaji.

Marekani ina wasiwasi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Ned Price jana aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba wana wasiwasi na taarifa za kuongezeka kwa ghasia dhidi ya waandamanaji nchini Sudan.

Price amesema Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayehusika na masuala ya Afrika, Molly Phee na mjumbe maalum wa Marekani katika Pembe ya Afrika aliyeteuliwa hivi karibuni, David Satterfield wanaelekea Sudan na watarejea wito wao kuvitaka vikosi vya usalama kumaliza ghasia na kuheshimu uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani.

Huku hayo yakijiri wanaharakati wa Sudan wameitisha siku mbili za uasi kuanzia siku ya Jumanne baada ya raia saba kuuawa Jumatatu kwenye maandamano. Aidha, madaktari wa Sudan wametangaza mgomo mkubwa na wamesema wanajiondoa kwenye hospitali za kijeshi kutokana na mauaji hayo.

(AFP)