1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya wanaharakati wa mazingira kuandamana kwa siku 3

15 Septemba 2023

Maelfu ya wanaharakati wa mazingira duniani kote wamepanga kufanya maandamano kuanzia leo hadi siku ya Jumapili ili kushinikiza viongozi wa dunia kuchukua hatua za kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabia nchi.

https://p.dw.com/p/4WN8h
Fernando Aguilar kutoka El Salvador akiwa amembeba mwanae wakijimwagia maji ili kupoza mwili kutokana na joto kali, Juni 18,2023.
Fernando Aguilar kutoka El Salvador akiwa amembeba mwanae wakijimwagia maji ili kupoza mwili kutokana na joto kali, Juni 18,2023. Picha: Adrees Latif/REUTERS

Maandamano hayo yananuia kushinikiza kuondokana na matumizi ya nishati ya kisukuku hasa wakati huu ambapo dunia inakabiliwa na majanga ya kiasili na ongezeko la joto.

Maandamano hayo, yaliyopangwa na mashirika ya kikanda na kimataifa ya mazingira likiwemo vuguvugu la mwanaharakati kijana Greta Thunberg la Friday for Future, yatafanyika katika nchi 50 na miji mbalimbali duniani na yataendelea hadi siku ya Jumapili.

Wiki iliyopita, Umoja wa Mataifa ulionya kuwa mataifa bado yako nyuma kufikia lengo la kupunguza ongezeko la joto duniani hadi nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Celcius, kulingana na ahadi ya kimataifa iliyotolewa mwaka 2015 chini ya mkataba wa Paris wa hali ya hewa.