1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Vyama vya siasa Ufaransa kuungana kukizuia chama cha Le Pen?

1 Julai 2024

Vyama vya siasa za wastani nchini Ufaransa vimekua mbioni kuungana kwa lengo la kukizuia kuwa na wingi wa viti bungeni chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha National Rally (RN) kinachoongozwa na Marine Le Pen.

https://p.dw.com/p/4hkP6
Ufaransa - Eric Zemmour (Resistons), Emmanuel Macron (LREM), Marine Le Pen (RN)
Wanasiasa wa Ufaransa: Kutoka kushoto Eric Zemmour (Resistons), Emmanuel Macron (LREM) na Marine Le Pen (RN)Picha: Patrick Batard /abaca/picture alliance

Hatua ya vyama hivyo inajiri baada ya chama cha RN kupata mafanikio ya kihistoria kwa kushinda duru ya kwanza ya uchaguzi wa Bunge.

Matokeo rasmi yaliyotangazwa jana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa yalikipa ushindi chama cha RN cha Le Pen asimilia 33 ya kura, kikifuatiwa na kundi la vyama vya mrengo wa kushoto lililojipatia asilimia 28 huku vyama vya siasa za wastani ikiwemo kile cha Rais Emmanuel Macron cha Muungano wa pamoja kikipata asilimia 20 tu ya kura.

Matokeo hayo yamekuwa pigo kubwa kwa Macron ambaye alilazimika mwezi uliopita kuitisha uchaguzi wa mapema baada ya chama chake kupata matokeo mabaya katika uchaguzi wa Bunge la Ulaya.

Ufaransa | Marine Le Pen, Mwenyekiti wa chama cha RN
Mwenyekiti wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha National Rally (RN), Marine Le PenPicha: Yves Herman/REUTERS

Uwezo wa kuunda serikali kwa chama hicho cha RN, itategemea na mafanikio ya vyama vya siasa za wastani na vile vya mrengo wa kushoto katika azma yao ya kuungana katika duru ya pili ya uchaguzi na hivyo kumzuwia Le Pen kuwa na wingi wa viti bungeni.

Wagombea wa  chama cha National Rally (RN)  ambacho kimejengeka katika sera ya kuwapiga vita wahamiaji na kuipinga taasisi ya Umoja wa Ulaya, walipata matokeo mazuri katika mamia ya maeneo bunge kote nchini Ufaransa.

Viongozi wa vyama vya mrengo wa kushoto wa New Popular Front na kile cha siasa za wastani cha rais Emmanuel Macron, walidhihirisha siku ya Jumapali ishara ya muungano wao kwa kusema wagombea wao katika baadhi ya wilaya wangelijiondoa ili kutoa nafasi nzuri zaidi kwa mgombea pinzani kuweza kupata ushindi dhidi ya mgombea wa RN katika  duru ya pili ya uchaguzi huo wa Bunge , itakayofanyika Jumapili ijayo ya Julai 7.

mwanasiasa wa Ufaransa na Mwenyekiti wa chama cha LFI | Jean-Luc Melenchon
Mwanasiasa wa chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto cha "La France Insoumise" (LFI) Jean-Luc Melenchon.Picha: Louise Delmotte/AP Photo/picture alliance

Walakini, haikuwa wazi ikiwa makubaliano hayo yatatekelezwa na chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto cha "La France Insoumise" (LFI) kinachoongozwa na Jean-Luc Melenchon, ambacho pia ni mojawapo ya chama kikuu katika muungano huo wa New Popular Front. Mélanchon ni mwanasiasa maarufu wa upinzani nchini Ufaransa ambaye anayefahamika mno kwa uzungumzaji wake wa wazi ambao umekuwa ukiibua hamasa lakini wakati mwengine ukizusha hisia mseto.

Soma pia: Chama cha Le Pen chashinda duru ya kwanza ya uchaguzi wa Bunge

Waziri wa Fedha Bruno Le Maire, ambaye ni mshirika wa chama tawala cha Macron, alitoa wito kwa wapiga kura kupitia redio ya France Inter kutochagua mgombea wa LFI, akisema chama hicho ni hatari kwa taifa. Tofauti za kisera, mivutano na maslahi ya kisiasa vilivyopo baina ya vyama hivyo inahatarisha azma yao ya kuungana na kumzuia Le Pen kuwa na udhibiti wa Bunge.

Je, kuna hatari ya kushuhudia Ufaransa isiyotawalika?

Wafaransa wakipiga kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Bunge
Wafaransa wakipiga kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Bunge mnamo Juni 30, 2024Picha: Laurent Cipriani/AP Photo/picture alliance

Mchambuzi wa taasisi inayoshughulika na kura za maoni ya Ipsos Mathieu Gallard alihesabu kuwa duru ya kwanza ya uchaguzi imeacha uwezekano kwa vyama vya siasa kugombea jumla ya viti 306 kati ya 577 vinavyowaniwa katika Bunge la Kitaifa la Ufaransa, huku akisisitiza kuwa duru ya pili imegubikwa na hali ya kutokuwa na uhakika wa chama gani kitaibuka na ushindi.

Miaka kadhaa iliyopita, muungano huu dhidi ya chama cha RN cha Le Pen unojulikana kama "republican front" ulikuwa ukipata mafanikio makubwa, lakini wachambuzi wamekuwa na mashaka iwapo wapiga kura wa Ufaransa wataitikia wito wa wanasiasa hao.

Soma pia: Ufaransa: Chama cha National Rally mguu sawa kuchukua hatamu

Wachambuzi wengi wanahoji ikiwa muungano huo utashindwa kufikia lengo lao, ni namna gani Ufaransa itatawaliwa na sera za RN zinazoupinga Umoja wa Ulaya, ama ni vipi rais asiye na wingi wa viti bungeni ataweza kuongoza hadi mwaka 2027. Lakini pia watetezi wa haki za binaadamu wanaelezea pia wasiwasi wao kutokana na sera kali za chama cha Marine Le Pen kuhusiana na haki za wahamiaji na athari yake katika uchumi wa taifa hilo.

(Chanzo: AFP)