1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Odinga: Nimeanza mapambano ya kumuondoa Ruto madarakani

Shisia Wasilwa
23 Januari 2023

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga, amesema ameanza mapambano ya kumuondoa madarakani Rais William Ruto, hii ni baada ya kudai kuwa alikuwa na kura za kutosha katika uchaguzi uliopita 2022

https://p.dw.com/p/4Maw5
Kenia Oppositionsführer Raila Odinga
Picha: Shisia Wasilwa/DW

Akiwahutubia wafuasi wake jijini Nairobi, Odinga amedai kuwa alishinda kwenye uchaguzi mkuu uliopita kwa zaidi ya kura milioni mbili, akisema wamebaini hayo baada ya wataalamu wa data kuyachunguza matokeo hayo. 

Uwanja wa Kamkunji wenye historia ya kuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa ya siasa nchini Kenya, ulianza kufurika wafuasi wa kiongozi huyo wa upinzani mapema asubuhi, huku wakimsubiri Odinga ambaye amekuwa Afrika Kusini tangu Januari 13, katika majukumu yake kama mjumbe wa juu wa Umoja wa Afrika kwa ajili maendeleo ya miundombinu.

Soma zaidi: Odinga akataa kuutambua ushindi wa Ruto

Mkutano huo na wafuasi wake, unafanyika siku chache baada ya kile kinachotajwa kuwa ufichuzi kuwa, Odinga alimshinda Rais Ruto kwenye uchaguzi mkuu uliopita, huku Raila akizoa kura milioni nane, na Ruto akipata kura milioni tano. Raila aliyeonekana mwenye ghadhabu amesema kuwa hataogopa chochote kwenye azma yake baada ya kunyang’anywa ushindi kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Kenia Oppositionsführer Raila Odinga
Kiongozi wa upinzani Kenya, Raila Odinga akiwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa katika uwanja wa KamkunjiPicha: Shisia Wasilwa/DW

Hata hivyo, matokeo rasmi ya Tume ya Kusimamia Uchaguzi na Mipaka, IEBC yalionesha kuwa Ruto alipata kura milioni 7.18 huku Odinga akipata kura milioni 6.94 na kusababisha Ruto kutangazwa mshindi. Raila amesema kuwa hapana haja ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwaka 2027, hadi uchafu kwenye uchaguzi usafishwe.

Desemba, 2022 muungano wa Azimio la Umoja uliahidi kuandaa maandamano kadhaa kuhusu kuongezeka kwa gharama za maisha, kutimuliwa kwa makamishna wanne wa  IEBC na kushindwa kwa serikali ya Kenya Kwanza kutimiza ahadi zake ilizozitoa wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu.

Odinga awataka Wakenya kususia kulipa kodi

Kiongozi huyo wa upinzani pia amewataka Wakenya kususia kulipa kodi ambayo imeongezeka maradufu tangu kuingia kwa utawala wa Rais Ruto. Hata hivyo, rais wa Kenya amesema hatokubali watu wachache wakwamishe utendaji wa kazi wa serikali yake ya kuwahudumia Wakenya.

Raila Odinga ameinyooshea kidole idara ya mahakama akidai kuwa serikali inaongozwa na wezi, kwani maafisa wakuu serikalini wamekuwa wakifutiwa makosa na mahakama.  Kwa sasa upinzani unataka matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita yakaguliwe upya na kutangazwa kwa Wakenya. Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa Muungano wa Azimio la Umoja, akiwemo Martha Karua, Kalonzo Musyoka, na kiongozi wa chama cha Roots George Wajackoya.