1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaendeleza mashambulizi katika kiwanda cha Azovstal

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
5 Mei 2022

Ukraine yasema Urusi imepania kuwaangamiza wanajeshi wake waliokuwa wamejificha katika kiwanda cha chuma cha Azovstal katika mji wa Mariupol.

https://p.dw.com/p/4Ar7b
Ukraine Krieg Azovstal in Mariupol
Picha: Alexei Alexandrov/AP Photo/picture alliance

Jeshi la Ukraine limeripoti juu ya mashambulizi hayo mapya yanayofanywa na vikosi vya Urusi kwenye kiwanda hicho cha chuma cha Azovstal kilichopo kwenye mji wa pwani wa Mariupol kaskazini mwa Ukraine. Mkuu wa jeshi la Ukraine amesema majeshi ya Urusi yanafanya mashambulizi hayo huku yakisaidiwa na kikosi cha anga, lengo kuu likwa ni kuchukua udhibiti wa eneo hilo la kiwanda. Urusi kwa upande wake imetangaza hatua ya kusitisha mapigano kwa saa kadhaa wakati wa mchana kila siku ili kuruhusu raia waliokuwa wamejihifadhi katika kiwanda hicho kwenda mahala salama.

Kushoto: Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron. Kulia: Waziri Mkuu wa India Narendra Modi.
Kushoto: Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron. Kulia: Waziri Mkuu wa India Narendra Modi.Picha: Mustafa Yalcin/AA/picture alliance

Wakati huo huo, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi katika taarifa yao ya pamoja baada ya kukutana mjini Paris kwa mazungumzo na chakula cha jioni hapo jana walitoa wito wa kusimamishwa mara moja uvamizi nchini Ukraine, huku Waziri Mkuu wa India akiepuka kulaani waziwazi uvamizi wa Urusi dhidi ya jirani yake Ukraine.

India, ambayo inaagiza vifaa vyake vingi vya kijeshi kutoka Urusi, kwa muda mrefu inaufuatilia mvutano kati ya nchi za Magharibi na Urusi kwa njia za kidiplomasia na ilikataa kuishutumu serikali ya Urusi na hata kupiga kura dhidi yake katika Umoja wa Mataifa. Ufaransa na India zimeonyesha wasiwasi mkubwa juu ya mzozo wa kibinadamu na vita vinavyoendelea nchini Ukraine.

Watoto wakimbizi kutoka Ukraine
Watoto wakimbizi kutoka UkrainePicha: Jelena Djukic Pejic/DW

Ofisi inayoshughulikia maswala ya uhamiaji na wakimbizi nchini Ujerumani imesema zaidi ya raia 600,000 wa Ukraine wanaokimbia vita nchini mwao wamewasili nchini humo tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mnamo Februari 24. Katika ya idadi hiyo, takriban asilimia 40 ya wakimbizi hao wa Ukraine ni watoto.

Taarifa zaidi zinafahamisha kwamba Urusi pia imefanya mazoezi ya silaha za nyuklia. Urusi imesema vikosi vyake hapo jana vilifanya mazoezi hayo ya nyuklia ingawa havikutumia makombora halisi ya nyuklia katika eneo la Kaliningrad kwenye Bahari ya Baltic. Eneo hilo lipo katikati ya nchi mbili wanachama wa Umoja wa Ulaya, Poland na Lithuania ambazo pia ni wanachama wa muungano wa kijeshi wa NATO.

Rais wa urusi Vladmir Putin
Rais wa urusi Vladmir PutinPicha: Kremlin Press Service/Handout/AA/picture alliance

Rais wa Urusi, Vladimir Putin amewahi kutoa vitisho akiashiria nia ya kuzitumia silaha za nyuklia tangu na kuonya juu ya kulipiza kisasi haraka iwapo nchi za Magharibi zitaingilia kati moja kwa moja vita kati ya nchi yake na Ukraine.

Vyanzo: AFP/AP/ https://p.dw.com/p/4Aq31