1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Vita vya Sudan vyatinga mwezi bila matumaini ya kumalizika

15 Mei 2023

Vita vya kuwania madaraka vimetimiza mwezi mmoja tangu vilipoanza, huku mapigano yakiendelea kuutikisa mji mkuu Khartoum.

https://p.dw.com/p/4RMIr
Sudan Khartum Rauch
Picha: AFP

Nayo mazungumzo ya amani yanayoendelea mjini Jeddah nchini Saudi Arabia bado hayajazaa matunda ya kusitisha vita kabisa.

Wasemavyo wenye busara wapiganapo mafahali wawili ziumiazo ni nyasi.

Katika muktadha wa mapigano nchini Sudan, nyasi ni familia na raia wa nchi hiyo ambao wanazidi kuteseka kutokana na vita kati ya majenerali wawili wanaohasimiana.

Mashambulizi yaendelea Khartoum wakati wapinzani wakikutana Saudia

Kwa mwezi mmoja sasa raia wamekuwa wakijaribu kukwepa risasi na kukimbilia usalama, uhaba wa vyakula na mahitaji mengine ya msingi umeendelea kukithiri. Umeme unakatika kila mara. Mawasiliano yanatatizika na mfumuko wa bei pia umepanda.

Kwa muda mrefu mji wa Khartoum wenye wakaazi milioni tano na ulioko karibu na Mto Nile, ulikuwa tulivu na tajiri, hata katika miongo ya vikwazo dhidi ya aliyekuwa rais wa zamani wa kiimla wa taifa hilo Omar al-Bashir.

Mji wa Khartoum wageuka kama mahame

Lakini sivyo tena. Kwa sasa, mji huo ni kama mfano tu wa mahame huku Mashambulizi ya makombora na ya angani yakiendelea kuzikumba sehemu mbalimbali.

Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, anayeongoza jeshi la taifa Sudan.
Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, anayeongoza jeshi la taifa Sudan.Picha: El Tayeb Siddig/REUTERS

Katika uwanja wa ndege wa Khartoum Khartoum ni mabaki ya ndege iliyoteketezwa moto. Kwenye mitaa ya Khartoum ni ofisi ambazo zimefungwa za ubalozi wa nchi mbalimbali, hospitali zilizoharibiwa, maduka na mabenki ambayo yamefungwa pamoja na maghala ya nafaka ambayo yameporwa.

Ndiyo taswira unayokumbana nayo ambayo imesababishwa na vita vilivyoanza Aprili 15, kati ya jeshi la taifa linaloongozwa na jenerali Abdel Fattah al-Burhan na naibu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo, anayekiongoza kikosi chenye nguvu cha wanamgambo Rapid Support (RSF).

Human Rights Watch yalaani matumizi ya silaha nzito Sudan

Kulingana na shirika linalofuatilia machafuko yanayohusisha silaha kama bunduki (Armed Conflict Location and Event Data Project) mapigano hayo tayari yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 750. Maelfu Zaidi pia wamejeruhiwa na tayari takriban watu milioni moja wameyakimbia makwao. Wengine wakikimbilia nchi Jirani kama Misri, Ethiopia, Chad na Sudan  Kusini.

Machafuko hayo yamewaacha kwenye mateso zaidi ya raia milioni 45, wa nchi hiyo ambayo ni kati ya mataifa maskini zaidi ulimwenguni.

Jenerali Mohamed Hamdan Daglo anayeongoza kikosi cha wanamgambo RSF
Jenerali Mohamed Hamdan Daglo anayeongoza kikosi cha wanamgambo RSFPicha: Akuot Chol/AFP

Mazungumzo ya amani hayajazaa matunda

Mikataba kadhaa ya kusitisha vita ilifikiwa hapo mwanzo lakini ilkiukwa na kuvunjika. Hata sasa mazungumzo kati ya wawakilishi wa pande hizo mbili yanaendelea mjini Jeddah nchini Saudi Arabia kutafuta suluhisho la kusitisha vita na kuruhusu misaada ya kiutu kupelekewa watu ambao wameathiriwa.

Pande hasimu Sudan zasaini makubaliano ya kuwalinda raia

Lakini matumaini ya kupatikana ufumbuzi ni hafifu na kila kukicha yanazidi kudidimia kufuatia hatua na kauli za pande zote.

Kila upande umeshutumiwa kwa kuvunja makubaliano kiholela, katika kiwango ambacho si cha kawaida.

Katika tukio la hivi karibuni zaidi, Jenerali Burhan ametangaza kutaifisha mali ya wanamgambo wa RSF. Naye hasimu wake, Jenerali Daglo amerekodi taarifa kwenye ukanda wa sauti akisema, Burhan atakabiliwa kisheria na kunyongwa mbele ya umma.

(Chanzo: AFPE)