Pande hasimu Sudan zasaini makubaliano ya kuwalinda raia
12 Mei 2023Usiku wa kuamkia leo Ijumaa kumetolewa taarifa za kutia moyo kuhusu mzozo wa Sudan. Duru zimearifu kuwa pande hasimu kwenye mzozo huo zimekubaliana kuwalinda raia na kuhakikisha huduma za msaada wa kiutu zinafika kwenye maeneo yenye uhitaji bila vizingiti.
Licha ya hatua hiyo, pande hizo mbili hazijakubaliana bado kusitisha mapigano wala kutafuta mkataba mpana wa kumaliza vita.
Maafisa wa Marekani waliokaririwa na Shirika la Habari la Associated Press wamesema maafikiano ya kumaliza vita ni jambo ambalo bado haliko karibu.
Baada ya wiki nzima ya majadiliano katika mji wa mwambao wa Jeddah nchini Saudi Arabia, kile kilichopatikana ni pande hizo mbili hasimu kutia saini azimio la kuonesha dhamira ya kufanya kazi pamoja ili kupata makubaliano mapya ya kusitisha vita kwa muda mfupi.
Azimio hilo linatilia mkazi umuhimu wa kila upande kusaidia upatikanaji huduma muhimu za kiutu na kuwalinda raia. Pia linatoa mwito wa kurejeshwa huduma ya nishati ya umeme, maji na nyingine muhimu.
Vikosi vya pande hasimu pia vinatakiwa kuondoka kutoka kwenye majengo ya hospitali na kila upande uruhusu kufanyika mazishi ya heshima kwa wale waliopoteza maisha.
Makubaliano ya kusitisha vita bado ni safari ndefu
Afisa mmoja wa Marekani anayeshirika mazungumzo hayo ameliambia shirika la habari la AFP azimio hiyo siyo la kusitisha vita na badala yake ni dhamira ya kila upande kulinda na kueshimu wajibu wao kwa sheria za kimataifa za utoaji msaada wa kiutu katika uwanja wa mapambano.
"Tunatumai, japo kwa tahadhari , kwamba dhamira yao ya kutia saini nyaraka hii itafungua nafasi itakayowalazimisha kuweka mazingira ya kuingiza mahitaji ya kibinadamu", amesema Afisa huyo wa Marekani ambaye jina lake halikutajwa.
Kulingana na maafisa wanaohudhuria mazungumzo ya mjini Jeddah, pande mbili hasimu ambazo ni Jeshi la Sudan na Kikosi cha Wanamgambo wenye nguvu cha RSF wangali wana tofauti kubwa juu ya jinsi mzozo unaoendelea unaweza kufikia mwisho.
Hali hiyo huenda imewafadhaisha wapatanishi kutoka Marekani na Saudi Arabia walioweka lengo la kufikia mkataba wa kusitisha mapigano ndani ya siku kumi za mazungumzo.
Licha ya mafanikio kidogo yalitangazwa kutokea Jeddah, nchini Sudan kwenyewe mapambano yameendelea kuripotiwa kutwa nzima ya jana Alhamisi na usiku wa kuamkia leo.
Mapigano yaliutikisa mji wa Halfaya, ambao ni lango la kuingia mji mkuu Khartoum. Wakaazi wa eneo hilo wamesema walisikia milio ya ndege za kivita ikizizima mjini Khartoum na kwenye miji pacha ya Bahri na Omdurman.
Licha ya rapsha hizo taarifa zinaeleza mapigano ya jana hayakuwa makali ikilinganishwa na ya siku ya Jumatano.
Baraza la Haki za Binadamu lataka mbinyo uongezwe kwa pande za hasimu Sudan
Katika hatua nyingine, hapo jan Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa liliandaa mkutano maalum maalum kuhusu machafuko yanayoendelea Sudan
Mkuu wa haki za binadamu la Umoja wa Mataifa Volker Turk alitumia mkutano huo wa mjini Geneva, kuirai jamii ya kimataifa kutumia njia zote zinazowezeka kuongeza mbinyo kwa pande zinazohasimiana Sudan ili kumaliza machafuko hayo.
Turk alikumbusha kuwa machafuko hayo yamewatumbukiza Wasudan wengi katika mgogoro na mateso.
Mbele ya macho ya umma, pande hasimu hazioneshi hadi sasa utayari wa kusalimu amri ili kumaliza mzozo huo uliozuka ghafla mwezi uliopita.
Mapigano hayo yanatishia kuitumbukiza Sudan kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe tayari yamesababisha vifo vya mamia ya watu na kuzusha hali ngumu ya kibinadamu nchini humo.
Makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano yalikiukwa kila wakati na kuwaacha raia wakitaabika katikati ya wimbi la hujuma za kila upande.
Miundombinu muhimu kama umeme na mifumo ya maji imelengwa na mashambulizi. Upatikanaji chakula umekuwa wa taabu na mfumo wa kutoa matibabu umeparaganyika.