1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita kusitishwa kwa muda mashariki mwa Kongo

5 Julai 2024

Marekani imepongeza usitishaji mapigano kwa wiki mbili mashariki mwa Kongo kuruhusu kupelekwa kwa msaada wa kiutu. Wakati huo huo UN imeelezea hofu juu ya kuongezeka kwa ulanguzi wa binadamu mashariki mwa Kongo.

https://p.dw.com/p/4huLg
DR Kongo Kibumba 2022 | Waasi wa M23
Wapiganaji wa kundi la waasi la M23 wakiwa wamesimama na silaha zao huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Disemba 23, 2024 Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Ikulu ya Marekani ya White House imesema makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yatakayoanza kutekelezwa leo Ijumaa kuanzia saa sita usiku na kuendelea hadi Julai 19, yatayahusisha maeneo ambayo migogoro huwaathiri zaidi raia.

Marekani yasema mashirika ya msaada yanashindwa kufikia eneo la mgogoro

Katika taarifa, msemaji wa baraza la usalama la kitaifa la Marekani Adrienne Watson, amesema kuongezeka kwa mapigano katika siku za hivi karibuni zaidi katika jimbo laKivu Kaskazini kumewazuia wafanyakazi wa mashirika ya msaada kufikia maelfu ya wakimbizi wa ndani katika eneo karibu na Kanyabayonga na kusababisha zaidi ya watu 100,000 kuyakimbia makazi yao.

Kongo na Rwanda zaunga mkono usitishaji vita mashariki mwa Kongo

Watson ameongeza kuwa serikali za Kongo na Rwanda zilielezea kuunga mkono makubaliano hayo ili kupunguza mateso kwa watu walio katika mazingira magumu na pia kuweka masharti kwa ajili ya kupunguza kwa kiasi kikubwa mvutano mashariki mwa Kongo.

Wakimbizi wa ndani katika kambi ya wakimbizi viungani mwa Goma, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wakikusanyika katika eneo la mlipuko kambini humo mnamo Mei 3, 2024
Wakimbizi wa ndani katika kambi ya wakimbizi viungani mwa Goma, Jamhuri ya Kidemokrasi ya KongoPicha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Taarifa hiyo imesema Marekani inatoa wito kwa pande zote kuheshimu makubaliano hayo.

Eneo la Kivu Kaskazini limekuwa likipambana na uasi wa kundi la M23 kwa zaidi ya miaka miwili pamoja na vurugu nyingine za makundi ya wapiganaji.

Mara kwa mara, Kongo,Umoja wa Mataifa na mataifa ya Magharibi yameishutumu Rwanda kwa kuliunga mkono kundi hilo la M23 kwa msaada wa wanajeshi wake pamoja na silaha, madai yanayokanushwa na nchi hiyo.

Ulanguzi wa binadamu mashariki mwa Kongo waibua hofu

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa walioidhinishwa na Baraza la Haki la Umoja wa Mataifa, wameelezea kushangazwa na idadi iliyoripotiwa ya takriban wahanga 531 wa unyanyasaji wa kijinsia unaohusishwa na migogoro kutoka Agosti 2023 hadi Juni 2024, katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Ituri, Tanganyika na Maniema.

Soma pia: Wanamgambo waua takriban watu 23 mashariki mwa DRC

DR Kongo Mugunga 2013 | Wanawake wakiwa kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani
Baadhi ya wanawake na wasichana walitekwa na wanamgambo ili kutumikishwa kingono wakati wakiwa katika harakati za kutafuta maishaPicha: Habibou Bangre/AFP/Getty Images

Wataalamu hao wamesema tuhuma zilizowasilishwa kwao, zinaelezea kuhusu wanawake na wasichana waliotekwa nyara kwa madhumuni ya ukatili wa kijinsia au unyanyasaji wa kingono, wakati wakitafuta chakula au kuni au kushiriki katika shughuli za kilimo.

Wataalamu hao wameongeza kuwa ripoti za kuhusika kwa vikosi vya ulinzi na usalama zinaibua wasiwasi mkubwa.

Wataalamu wa UN waelezea hofu ya kuondoka kwa MONUSCO Kongo

Wataalamu hao pia wameelezea wasiwasi kuhusu kukatizwa kwa operesheni ya Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, MONUSCO.

Wameelezea wasiwasi wao kwamba kwa kuondoka kwa kikosi hicho, masuala muhimu ya mifumo ya tahadhari ya mapema ya ukiukaji wa haki za binadamu hayatakuwepo.

Soma pia:Kikosi cha MONUSCO chaondoka rasmi Kivu Kusini

Hivi karibuni, ujumbe wa MONUSCO ulijiondoa kutoka jimbo la Kivu Kusini na unatazamiwa kuondoka Kivu Kaskazini na Ituri, majimbo mawili ya mwisho ambapo bado ujumbe huo unatekeleza majukumu yake ijapokuwa tarehe bado haijatajwa.