1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita Gaza ni mtaji wa kisiasa kwa watalawala wa kiimla?

2 Septemba 2024

Vita vya Gaza vimegeuka kuwa mtaji wa kisiasa kwa watawala wa kiimla katika Mashariki ya Kati kama vile Abdel Fatah el-Sisi wa Misri na wengine.

https://p.dw.com/p/4kBgu
Israel, Ukanda wa Gaza | Kifaru kikiwa katika uwanja wa vita
Kifaru cha Israel kikiwa katika eneo la uwanja wa vitaPicha: Amir Cohen/REUTERS

Katika siku za hivi karibuni, baada ya mashambuliano makubwa ya makombora kati ya Israel na Hezbollah, kiongozi wa Misri Abdel-Fattah el-Sissi alizungumza na mmoja wa majenerali wakuu wa Marekani, ambapo alitahadharisha juu ya hatari ya kuongezeka zaidi kwa mgogoro wa Gaza.

Rais huyo wa Misri amesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kufanya juhudi zote na kuongeza shinikizo ili kuepusha kuongezeka kwa uhasama unaotishia usalama na utulivu wa eneo la Mashariki ya Kati.

Rais el-Sisi amesema hayo baada ya ziara ya jenerali wa Marekani, Charles Quinton Brown nchini Misri .Kiongozi wa Misri alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya Israel na wapiganaji wa Hezbollah kushambuliana.

Pamoja na Marekani na Qatar, Misri ni sehemu ya wajumbe wa wapatanishi wanaojaribu kufanya mazungumzo juu ya kusimamisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza, ambako Israel imeendeleana operesheni yake ya kijeshi tangu Hamas walipofanya mashambulio ya Oktoba 7.

Kauli hizo zinamsaidia el-Sissi kuijenga haiba yake. Hayo ameyasema Hossam el-Hamalawy, mtafiti na mwanaharakati wa Misri anayeishi nchini Ujerumani ambaye anaandika jarida linaloangazia siasa za Misri.

Soma pia:Wafanyakazi Israel wagoma baada ya kuuawa mateka

Mtafiti huyo ameeleza kwamba vita vya Gaza kimsingi vimesaidia kuimarisha zaidi utawala wa el-Sisi. Vita hivyo vya Gaza vimekuwa njia ya Misri ya kuingiza vipato baada ya sekta za utalii na usafirishaji wa meli kukwama.

Kutokana na hali hiyo Marekani na Umoja wa Ulaya zinajibiidisha kuinusuru Misri. Vitega uchumi thamani ya dola bilioni 50 vimewekezwa nchini Misri ambavyo vimeiwezesha  sarafu ya Misri, kuepuka kusambaratika.

"Vita vya Gaza kimsingi vimesaidia kuimarisha utawala wa el-Sissi hata zaidi. Utawala huu ambao kwa miaka michache iliyopita umelegalega katika nyanja ya utawala, na umeshindwa katika nyanja ya Uchumi hatua ambayo imeiingiza nchi katika kiwango cha kutisha cha deni ambacho hakijawahi kuonekana katika historia ya Misri." Alisema El-Hamalawy.

Aliongeza kwamba kutokana na kuzuka kwa vita, hata ingawa wakati mwingine hali hii imetishia utulivu wa nchi pamoja na maandamano ya hapa na pale yaliyotokea mwanzoni mwa vita ambayo yalizimwa kikatili –

"hali hii imemsaidia el- Sisi kuimarisha utawala wake kutokana na Marekani na mataifa mengine yenye nguvu ya duniani kukimbilia kumwokoa kwa kutangaza fedha kutolewa zaidi ya dola bilioni 57 kwa Misri mwaka huu katika miezi michache iliyopita."

Vita vya Gaza ni silaha kwa wapindani wa ndani

Mtafiti al-Hamalawy amesema rais el-Sisi anakwenda nchi za magharibi kusema kwamba anapambana na ugaidi na kwa hivyo yeye ni muhimu kwa utulivu wa Mashariki ya Kati. Lakini wakati huo huo anawakandamiza wapinzani wa ndani ya nchi yake.

Amesema miongoni mwa waliokamatwa hivi karibuni ni Ashraf Omar, mchoraji wa vibonzo. Msanii huyo anashilikiwa kwa sababu ya vibonzo anavyochora. Anashikiliwa kwa tuhuma za ugaidi kama ilivyo kwa waandishi wengine wa habari wa Misri na wafanyakazi wa vyombo vya habari kwa jumla.

Israel yazidisha mashambulizi katika ukanda wa Gaza

El-Sissi anatumai kuona hasira za wananchi zikielekezwa kwa Israel na pia kwa Marekani kwa sababu ya kuwaunga mkono waisraeli katika vita vya Gaza.

Alia Brahimi na Karim Mezran watafiti waandamizi katika Baraza la Atlantiki, waliandika katika chapisho la taasisi yao la mwezi Julai kwamba el-Sisi si mtawala pekee katika Mshariki ya Kati anayenufaika na vita Gaza.

Soma pia:Waisraeli waanzisha mgomo wakishinikiza kuachiliwa kwa mateka

Wamesema watawala wa Algeria,Tunisia, Libya na Morocco pia wameweza kutumia masuala ya vita, wakimbizi, migogoro ya kimataifa na siasa za hamasa barani Ulaya kwa lengo la kunusuru uchumi wa nchi zao.

Algeria imeutumia mgogoro wa Gaza, kwenye baraza la usalama la Umaoja wa Mataifa kuonesha mshikamano na nchi za kiarabu. Lakini wakati huo huo Algeria inawaandama wanaharakati wanaotetea demokrasia na haki za binadamu nchini humo.

Nchini Tunisia, wanaharakati wanasema rais Kais Saied amekuwa akitumia msimamo wa kuiunga mkono Palestina kuwavuruga raia kutokana na mzozo wa kiuchumi huku akiendelea kuukandamiza upinzani nchini Tunisia.

Marc Lynch, profesa wa sayansi ya siasa na masuala ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha George Washington, amesema haamini kwamba mambo yanaweza kuendelea hivi. Amesema, tawala zinatakiwa kuwa makini zaidi katika kujibu masuala kama vile vita vya Israel na Wapalestina.