1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Visa 56 vya COVID-19 kwenye gereza la kijeshi nchini Congo

Saleh Mwanamilongo
4 Mei 2020

Serikali ya Congo imesema wafungwa wote walioko katika gereza la kijeshi la Ndolo,jijini Kinshasa wataendelea kubaki humo.Hatua hiyo imefuatia kuripotiwa visa 56 vya wafungwa walioambukizwa na virusi vya Corona.

https://p.dw.com/p/3bkRH
Rais wa Congo Felix Tshisekedi akiongoza kikao cha dharura jinini Kinshasa katika kupambana na Corona
Rais wa Congo Felix Tshisekedi akiongoza kikao cha dharura jinini Kinshasa katika kupambana na CoronaPicha: G. Kusema

Serikali ya Congo imesema wafungwa wote walioko katika gereza la kijeshi la Ndolo, jijini Kinshasa wataendelea kubaki humo. Hatua hiyo imefuatia kuripotiwa visa 56 vya wafungwa walioambukizwa na virusi vya Corona. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanaelezea wasiwasi wao kuhusu hatua hiyo ya serikali ambayo inahatarisha maisha ya wafungwa hao kutokana na kile yanachoelezea kuwa ni huduma mbovu pamoja na misongamano katika magereza ya Congo.

Kufuatia kikao cha dharura baina ya waziri mkuu Sylvestre Ilunga na mawaziri wa sheria na yule wa afya,serikali ya Congo imeelezea kwamba hatua zimechukuliwa ili kuwapa huduma bora wafungwa kwenye gereza la kijeshi la Ndolo, lakini wafungwa hao wataendelea kubaki rumande. Waziri wa Congo wa Afya, Eteni Longondo amesema kwamba wafungwa wote walioambukizwa hivi sasa wamewekwa kwenye karantini.

''Hatua tuliyoichukuwa ni kwamba tutawapima wafungwa wote ili kufahamu idadi rasmi ya walioambukizwa na virusi vya Corona. Pili tutaweka mahema kwenye uwanja wa gereza hilo ili kuwatenganisha wale walioambukizwa na wale ambao bado hawaja ambukizwa.Lakini wafungwa wote wataendelea kubaki humo humo'' alisema Dr Eteni.

Gereza hilo la kijeshi lenye ulinzi mkali,linawafungwa wapatao 2,000 na mashirika ya kutetea haki za binadamu yanaelezea kamba kuna msongamano mkubwa kwenye gereza hilo. Waziri wa afya amesema kwamba uchunguzi unabainisha mwanamke aliyemletea chakula mume wake ndiye aliyeuingiza ugonjwa huo kwenye gereza hilo.

Demokratische Republik Kongo l anhaltende Ebola-Epidemie
Picha: picture alliance/AP Photo/J. Delay

Serikali yatakiwa kuchuwa hatua za haraka

Wiki mbili zilizopita shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilielezea wasiwasi wake kuhusu hali ya wafungwa kwenye magereza ya Congo wakati huu wa mripuko wa Corona. Misongamano na huduma mbovu kwenye magereza ya Congo kunahatarisha maisha ya maelfu ya wafungwa nchini humo, lilielezea shirika hilo.

HRW inaelezea kwamba ni vigumu kutekeleza hatua za usafi na za kutosogeleana kwenye magereza ya Congo. Omar Kavota mratibu wa shirika la kutetea haki za binadamu la CEPADHO amesema kwamba serikali inatakiwa kuchukuwa hatua za haraka ili kuepusha visa vya maambukizi kwenye magereza.

''Hatua ya serikali ya kutaka hao wafungwa wabaki gerezani inaweza huenda inalenga kuwakinga jamii,lakini hata hivyo serikali ilitakiwa kuchukuwa mikakati iliwafungwa walioambukizwa na COVID-19 washughulikiwe vivilvyo''.

Kiasi cha asilimia 71 ya mahabusu nchini Congo bado wanasubiri kesi zao, na kuna zaidi ya wafungwa 500 waliohukumiwa adhabu ya kifo lakini toka mwaka 2003 Congo haijatekeleza adhabu hiyo.

Waziri wa sheria Celestin Tunda alisema mahabusu 1,200 katika gereza kuu la Kinshasa la MAKALA, ambao walifanya makosa madogo waliachiwa huru wiki iliyopita katika juhudi za kupambana na virusi vya Corona. Hadi kufikia sasa Congo imeripoti visa 652 vya Corona vikiwemo vifo 33.