1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa WHO wakutana Kongo kujadili Mpox

27 Agosti 2024

Shirika la Afya duniani, WHO, limesema litahitaji dola za Marekani milioni 135 katika kipindi cha miezi sita ijayo ili kukabiliana na mripuko wa ugongwa wa homa ya nyani unaosababishwa na virusi vya Mpox.

https://p.dw.com/p/4jxam
Mgonjwa wa Mpox Kivu Kusini
Mgonjwa wa Mpox Kivu KusiniPicha: Ruth Alonga/DW

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Gebreyesus alisema katika taarifa mjini Geneva Jumatatu, kuwa milipuko ya mpox katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na mataifa jirani inaweza kudhibitiwa na kuzuwiwa kabisaa, lakini kufanya hivyo kunahitaji mpango mpana na ulioratibiwa wa hatua.

Mpango wa Utayarifu na uitikiaji wa WHO uliozinduliwa Jumatatu, unatazamiwa kutekelezwa katika kipindi cha kuanzia Septemba 2024 hadi Februari 2025, na unakadiria mahitaji ya ufadhili wa dola milioni 135 kuutekeleza.

"Ni wazi kwamba mwitikio ulioratibiwa wa kimataifa ni muhimu kuzuwia milipuko hii na kuokoa maisha. Dharura ya kimataifa afya ya umma ndiyo ngazi y ajuu kabisaa ya tahadhari chini ya sheria ya kimataifa ya afya," alisema Gebreyesus.

Chanjo ya Mpox
Mgonjwa aliyeambukizwa mpox akipata matibabu Kivu KaskaziniPicha: Xinhua/IMAGO

Mwanzoni mwa mwezi huu wa Agosti, WHO ilitangaza dharura ya afya ya kimataifabaada ya kuongezeka kwa visa vya kirusi kipya cha Mpox nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambacho kimesambaa nje ya mipaka ya taifa hilo tangu wakati huo.

Mnamo Agosti 19, waziri wa afya nchini humo alisema walitarajia kupokea dozi za kwanza za chanjo ya mpox wiki hii, kufuatia ahadi kutoka Marekani na Japan.

Soma:  Kwanini chanjo za mpox zinawasili Afrika baada ya miaka 2

Lakini alipoulizwa iwapo Kongo itaanza kupokea dozi hizo wiki hii, mkuu wa kikosi kinachoshughulikia Mpox nchini Kongo, Cris Kacita, aliliambia shirika la habari la Uingereza Reuters, kuwa bado kuna michakato kadhaa ya kufuata.

Alisema mamlaka ya udhibiti wa dawa ya Kongo inahitaji kuwasiliana na kampuni ya Denmark inayotengeneza chanjo hiyo - Bavaria Nordic, kwa miongozo kabla ya chanjo kuwasili nchini humo, na kuongeza kuwa bado wanasubiri.

DR Kongo | Mpox | Kivu Kaskazini
Mripuko wa Mpox Kivu KaskaziniPicha: Ruth Alonga/DW

Bavaria Nordic, moja ya kampuni chache za dawa zilizo na chanjo ya mpox kwa sasa, ilisema katikati ya mwezi Agosti kwamba ilikuwa imekiarifu kituo cha kuzuwia na kupambana na magonjwa barani Afrika, CDC, kwamba inaweza kuzalisha dozi milioni 10 za chanjo kufikia mwishoni mwa mwaka 2025. Ilisema inaweza tayari kusambaza dozi milioni mbili mwaka huu.

Hapo jana serikali ya Ujerumani ilisema itatoa dozi 100,000 za chanjo hiyo kwa mataifa yanayoteseka na ongezeko la visa la mpox, ambazo ilisema zitatoka kwenye shehena ya jeshi lake na kutolewa katika kipindi cha muda mfupi.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Hebestreit, aliwambia waandishi habari kuwa lengo ni kuunga mkono juhudi za kimataifa za kudhibiti mpox barani Afrika. Hebestreit alisem Ujerumani pia itatoa msaada wa kifedha kwa WHO, pamoja na kuwasaidia washirika barani Afrika, kupitia muungano wa chanjo wa Gavi.