1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yashuhudia ongezeko la maambukizi ya mpox

Admin.WagnerD20 Agosti 2024

Maambukizi ya ugonjwa wa homa ya nyani, Mpox yanaongezeka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika wakati taifa hilo linasubiri chanjo za msaada kutoka Marekani na Japan.

https://p.dw.com/p/4jgKU
Chanjo ya mpox
Picha ikionyesha chanjo dhidi ya mpox. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeendelea kushuhudia ongezeko la maambukizi ya mpox, wakati ikisubiri chanjoPicha: PATRICK T. FALLON/AFP

Ripoti zilizotolewa na wizara ya afya hapa Kongo zinaonesha idadi ya wagonjwa waligundulika kuwa na homa ya Mpox imefikia 16,700 kutoka 16,000 siku chache zilizopita. Kwa jumla watu 570 wamekwishakufa kutokana na maradhi hayo.

Kutokana na athari hizo Waziri wa Afya Samuel Roger Kamba ametangaza baadhi ya hatua ili kupambana na kusambaa ugonjwa wa mpox.

Soma pia:Jamhuri ya Kongo yaripoti visa kadhaa vya homa ya nyani, mpox 

Hatua hizo ni pamoja na kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono, kuepuka ngono zembe, unadhifu wa mwili, kutokula nyama kibudu na kutowauguza wagonjwa.

"Lakini hatua muhimu ni ile ya chanjo. Tunawapa ifike hapa. Na tutakapoanza kuwapa watu chanjo, kipaumbele kitakuwa maeneo yaliyoathirika zaidi, maeneo tunayoyaita "hot-spot". Lakini inabidi chanjo hiyo inayouzwa kwa bei ghali imfikie yule anayeihitaji."

Kongo | Mpox
Mtumishi wa afya akimsaidia mgonjwa wa mpox katika kituo cha Munigi nchini Kongo, Agosti 19, 2024Picha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

Soma pia: WHO yasema ni muhimu kujiandaa kudhibiti kusambaa kwa mpox

Waziri Kamba amesema vijana ni waathirika wakubwa kwa kuwa wengi walizaliwa baada ya kusimamishwa kwa chanjo.

Alisema "Kabla ya 1980 watu walikuwa wanakingwa na chanjo. Ilikuwa tatizo kubwa na kilichosimamisha kusambaa kwa ndui ilikuwa ni chanjo peke yake. Lakini chanjo ilisimamishwa baada ya ugonjwa huo kutoweka. Ndio maana vijana waliozaliwa baada ya kipindi hicho, hawana kinga mwilini na ndio maana wanaambukizwa kiurahisi."

Soma pia: WHO yaitisha mkutano kuujadili ugonjwa wa homa ya nyani

Waziri huyo amesema chanjo hiyo inatarajiwa kuwasili wiki ijayo nchini humo na inatarajia kuwapatia chanjo watu zaidi ya milioni tatu. Japan na Marekani ndio wametangaza kuipatia Kongo chanjo hiyo.

Soma pia: Zaidi ya visa 18,700 vya mpox vyagunduliwa barani Afrika