1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa kidini Congo waunga mkono amani

21 Februari 2022

Viongozi wa dini huko Kivu ya Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameafikiana kuiunga mkono serikali katika juhudi za kusaka amani kwenye eneo hilo.

https://p.dw.com/p/47Kpu
Demokratische Republik Kongo Katholische Kirche Bischöfe
Picha: Giscard Kusema/Presidency of the Democratic Republic of the Congo

Eneo hilo liliwekwa chini ya utawala wa kijeshi tangu mwezi wa Mei mwaka jana. Viongozi hao wa kidini wameamua kuyatembelea maeneo yanayoathirika na vita vinavyoendeshwa na makundi ya waasi kusambaza ujumbe wa amani.

Kwa muda wa masaa matano viongozi hao kutoka dini za Kikristo na Kiislamu wamekuwa wakijadili kuhusu mikakati muafaka inayoweza kutumiwa kuhamasisha vijana kuachana na makundi ya waasi yanayoendelea kuwaua raia katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri mikao ambamo baadhi ya vijiji  vimeendelea kubaki na ukiwa.

DR Kongo | Nord Ost Ituri | Menschenrechtsverletzungen
Wanajeshi wakiwa katika eneo la Mashariki mwa KongoPicha: Tom Peyre-Costa/NRC

Akizungumza na waandishi wa habari, Wily Ngumbi Ngengele, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki mjini Goma, amebainisha kuwa ushirikiano huu ni njia pekee itakayoweza kuisaidia serikali ya Kongo kudumisha amani na usalama eneo lote la mashariki mwa Congo.

Kwa muda mrefu makanisa yamekuwa yakiingilia kati maswala ya kiusalama mashariki mwa Congo lakini bila mafanikio makubwa, huku kukiendelea kushuhudiwa ongezeko la makundi ya waasi ambao asilimia kubwa ni vijana waliopoteza matumaini ya kupata ajira.

Aidha, viongozi hao wa kidini wamedai kuwa sala pamoja na nyimbo zitatumiwa katika kipindi cha miezi mitano ya kutembelea maeneo yaliyoathirika kwa vita ili kuwaweka raia wote katika hali ya kuhimiza amani.

Kwa zaidi ya miongo miwili sasa raia wanaoishi katika vijiji vya ndani pamoja na mamia ya wengine wanaoishi katika wilaya ya Beni wameendelea kuwa wahanga wa mashambulizi yanayoendeshwa na makundi ya Mai Mai, likiwemo la ADF Nalu linalowaua raia kwa kuwakata kwa mapanga.

Haya yanajiri miezi michache tu baada ya ushirikiano wa jeshi la Kongo pamoja na Uganda kuanzisha mashambulizi makali dhidi ya ngome za waasi wa ADF Nalu katika wilaya ya Beni na kuanza kurejesha matumini ya amani kwa maelfu ya raia.