1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi kukutana karibuni kuhusu mashariki ya Kongo: Angola

28 Juni 2024

Angola imesema kuwa marais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda huenda wakakutana hivi karibuni kwa mazungumzo yenye lengo la kuleta amani katika eneo la mashariki ya Kongo linalokumbwa na machafuko.

https://p.dw.com/p/4hc78
Felix Tshisekedi | Joao Lourenco | Paul Kagame
Angola ni msuluhishi katika mzozo wa mashariki ya Kongo katika juhudi za kupata amani ya kudumuPicha: Arsene Mpiana/Michele Spatari/Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Rais wa Angola Joao Lourenco amesema wakati wa ziara yake Cote d'Ivoire kuwa mazungumzo yanaendelea kwa sasa, katika ngazi ya uwaziri, kwa lengo la kuwaleta pamoja wakuu wa nchi za Kongo na Rwanda, kwa mazungumzo ya ana kwa ana kuhusu haja ya kupata amani ya kudumu.

Lakini Waziri Mkuu wa Kongo Judith Suminwa Tuluka amefuta kuwepo mazungumzo yoyote na Rwanda, akitoa wito wa kuchukuliwa hatua kali na vikwazo dhidi ya Kigali.

Angola imekuwa msuluhishi katika mzozo wa eneo la mashariki ya Kongo la Kivu Kaskazini, ambako waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda wamekuwa wakipigana na vikosi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwishoni mwa mwaka wa 2021.

Juhudi za kidiplomasia zimekuwa zikiendelea kwa miezi kadhaa kuwaleta pamoja Rais Paul Kagame wa Rwanda na Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.