1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki: Erdogan asema mauaji ya Jamal Khashoggi yalipangwa

23 Oktoba 2018

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametoa maelezo ya kwanza rasmi juu ya mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul. Amesema mauaji hayo yalipangwa.

https://p.dw.com/p/3700h
Erdogan bei AKP-Sitzung im türkischen Parlament
Picha: Reuters/T. Berkin

Rais Erdogan alianza kwa kuwapa pole familia ya mwandishi Jamal Khashoggina raia wa Saudi Arabiakwa jumla kisha aliendelea kueleza yale yote yaliyotokea kabla na siku mwandihsi huyo alipofika kwenye ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul.

Amesema mpango wa mauaji hayo ulianza kuandaliwa mnamo tarehe 29 mwezi Septemba. Erdogan amesema kamera za ubalozini hapo ziliondolewa kabla ya mauaji hayo na siku moja kabla ya mauaji hayo wataalamu wa uchunguzi wa jinai waliwasili mjini Istanbul. mwandishi Jamal Khashoggi aliuawa tarehe 2 Oktoba. Erdogan pia amesema baada ya Khashoggi kuuawa mmoja wa watu hao alivaa nguo zake na kutoka ubalozini ili aonekane kuwa mwandishi huyo alitoka ubalozini hapo.

Rais Erdogan ameutaka utawala wa kifalme uwataje wote waliohusika na mauaji ya Jamal Khashoggi. Katika hotuba yake rais Erdogan amesema wauaji hao wa Saudi Arabia walirekodi kila kitu na ameuliza uko wapi mwili wa Jamal Khashoggi?. Wakati huo huo Erdogan ametaka washukiwa 18 waliokamatwa nchini Saudi Arabia waletwe Uturuki kujibu mashtaka ya kumuua Jamal Khashoggi.

Rais Erdogan pia amesema hatilii mashaka uadilifufu wa mfalme wa Saudi Arabia lakini anataka uchunguzi wa uwazi. Hotuba hiyo ya rais Erdogan ameitoa muda ambao utaonekana kuwa na utata zaidi kwa mrithi wa mfalme Mohammed bin Salman kutokana na mkutano wa uwekezaji, uliopewa jina la "Davos ya jangwani", ulioanza mjini Riyadh leo hii Jummane, ambao umegubikwa na kivuli cha mauaji ya Khashoggi baada ya wajumbe wakuu kujiondoa kwa maana kwamba hawahudhurii mkutano huo.

Mwandishi aliyeuawa Jamal Khashoggi
Mwandishi aliyeuawa Jamal Khashoggi Picha: picture-alliance/AP Photo/V. Mayo

Wafanyabiashara wengi, ikiwa ni pamoja na benki za Goldman Sachs na JP Morgan, viongozi wa Uber na Maafisa wa magharibi kama vile Mkuu wa Shirika la Fedha duniani Christine Lagarde wameususia mkutano huo wa uwekezaji wa siku tatu.

Kuuawa kwa mwandishi huyo wa gazeti la Marekani la Washington Post kumeharibu sifa ya kimataifa ya mrithi wa mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman ambaye anaongoza mpango wa mageuzi katika falme hiyo ya kiarabu.

Saudi Arabia ilithibitisha mauaji hayo ya Jamal Khashoggi baada ya zaidi ya wiki mbili tangu yalipotokea. Mauaji hayo yamesabbaisha shutuma na lawama kutoka kwa washirika wakubwa wa taifa hilo kutoka nchi za Magharibi. Rais wa Marekani Donald Trump amesema hakuridhika na maelezo yaliyotolewa na Saudi Arabia.

Kadhia hiyo inammulika bin Salman ambaye alisifiwa mno kwa kufanya marekebisho nchini mwake ikiwa ni pamoja na kuwapa wanawake haki ya kuendesha gari lakini sasa analaumiwa kuwa ameamuru mauaji ya Khashoggi, madai ambayo Saudia inayakataa kabisa.

Hata hivyo mkuu wa kampuni kubwa ya nishati Total ya nchini Patrick Pouyanne, amesema atahudhuria mkutano huo. Amesema siasa za domo kaya haziendelezi haki za binadamu.

Mwandishi:Zainab Aziz/DW/AFPE/APE

Mhariri: