1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utafiti: Watu 476 walifariki kutokana na UVIKO-19 Tanzania

Florence majani17 Agosti 2023

Utafiti mpya uliofanywa nchini Tanzania kuhusu hali ya UVIKO-19, umebaini kuwa watu 476 walifariki dunia kutokana na ugonjwa huo katika kipindi cha Januari 2021 hadi Desemba 2022, huku watu wengine 826 wameathirika.

https://p.dw.com/p/4VH07
Hygieneinstitut und Labor in Togo
Picha: Ute Grabowsky/photothek/picture alliance

Utafiti uliofanywa kati ya Wizara ya Afya, Hospitali za rufaa nchini ikiwamo Muhimbili na Hospitali ya rufaa ya  Bugando, na Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili, nchini Tanzania, umebaini kuwa, kati ya watu 1,783 waliougua ugonjwa wa UVIKO-19, katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2022, kati yao 476 ambao ni sawa na asilimia 40 walifariki dunia.

Hayo yameelezwa leo na Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani ya mwili na mapafu, Elisha Osati katika warsha ya wanasayansi na wanahabari, iliyoandaliwa na asasi ya kimataifa ya sayansi, AVAC .

Akizungumza katika warsha hiyo, Dk  Osati, amesema hawa ni wale wagonjwa ambao madaktari walipata taarifa zao kamili za kuugua UVIKO-19. Amesema wengi waliopoteza maisha ni wale waliokuwa na magonjwa mengine sugu kama vile virusi vya Ukimwi, kisukari, shinikizo la damu na wazee. 

Soma pia:Tanzania yalegeza masharti ya COVID-19

Dk Osati ameiambia DW kuwa UVIKO-19 ulileta madhara ya muda mfupi na ya kudumu kwani licha ya vifo hivyo, bado wapo wagonjwa 826 ambao wamebaki namadhara ya kudumu ikiwamo kubaki na makovu kwenye mapafu yao.

Utafiti huu umetolewa katika kipindi ambacho sasa watafiti wanaona kuna uhuru wa kuchapisha takwimu zao hali ambayo haikuwepo wakati wa uongozi wa awamu ya tano. Dk Osati anafafanua zaidi:

Wadau: Kuminywa kwa tafiti na taarifa huenda kumechangia

Akizungumzia umuhimu wa kutoa takwimu kwa wanahabari, Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Wanahabari nchini , UTPC Kenneth Simbaya ameiambia DW tafiti zinapominywa, zinazuia maendeleohasa katika sekta ya afya.

Maoni ya Watanzania juu ya Covid 19 na chanjo yake

Simbaya amesema awali tafiti kama hizi hazikutolewa hali iliyosababisha kuzuka kwa taharuki hasa kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwamo UVIKO-19.

Soma pia:Watanzania 80% walioambukizwa COVID-19 hawakuenda spitalini

Februari, mwaka 2021, Shirika la Afya Duniani, WHO liliionya Tanzaniakuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya UVIKO-19 wakati ambapo takwimu halisi za wanaougua ugonjwa huo hazikuwa zikitolewa kwa umma.

Katika kipindi hicho, vyombo vya habari na wanasayansi, wakiwamo madaktari hawakuwa pia wakitamka jina la ugonjwa huu hadharani bali waliutaja kama changamoto ya kupumua.