1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usalama wazidi kuzorota nchini Kongo

Admin.WagnerD13 Machi 2023

Wapiganaji wanaoshukiwa kutoka kundi la ADF wameua watu wasiopungua 17 kijiji cha Kirindera katika utawala wa Bashu siku chache tu baada ya waasi hao kufanya mauaji mengine katika eneo hilo linalokabiliwa na machafuko.

https://p.dw.com/p/4Oas9
Kongo | Demokratische Republik Kongo DRC Soldaten
Vikosi vya muungano vilivyopo nchini Kongo kupambana na makundi ya waasi Picha: Alain Uaykani/Xinhua/picture alliance

Mauwaji haya ya Kirindera yanafuatia yale ya Mukondi na Mausa katika utawala huo huo wa Bashu, ambako watu zaidi ya 40 waliuawa kwa mapanga, shoka na pia risasi juma lililopita. Mkazi wa Kirindera aliezungumza kwa njia ya simu na idhaa hii, alituambia walikoelekea waiganaji wa ADF, baada ya kufanya mauaji hao, pamoja na kuchoma moto hoteli moja, pikipiki pamoja na gari hapo Kirindera. 

Soma Zaidi:M23 wakabiliana na jeshi na kukaidi amri ya kusitisha mapigano Kongo 

Mlolongo wa mashambulizi katika utawala wa Bashu wilayani Beni, unadhaniwa na wengi kwamba utarudisha nyuma maendeleo kwenye utawala huo, ikiwa jeshi la serikali halitasuka mikakati ili kuwalindia usalama wakaazi wa vijiji pamoja na mali zao. Katembo Muhongya Agustin, ni mmoja wa wazee wa busara kwenye utawala wa Bashu. Amewaomba viongozi wa jeshi kufungua kambi muhimu ya wanajeshi Bashu, ili kuepusha mauaji siku za usoni.

Amesema, "Tunasikitika kuona kijiji kabambe hiki kuchomwa moto nakubaki majivu pekeake. Hii ni ishara ya maendeleo kufilisika katika kongamano letu. Kirindera kikiwa ni kijiji kikubwa, inabidi kuwekwa hapa kambi kubwa ya jeshi ilikuwalindia usalama wakaazi."

Demokratische Republik Kongo Flüchtlinge
Raia wengi nchini Kongo wanayakimbia maeneo yao kutokana na mashambulizi ya makundi ya waasi. Picha: Nicholas Kajoba/Xinhua/IMAGO

Mauaji yanayofanywa na ADF yanatajwa na wadadisi wa masuala ya usalama kuwa ni ya kulipiza kisasi cha mmoja wa makamanda wao muhimu Fezza Mulalo Seguja, aliyeuawa na majeshi ya muungano yaani UPDF na FARDC siku chache zilizopita.

Kwa mujibu wa msemaji wa operesheni za pamoja kati ya jeshi la Congo na lile la Uganda kanali Mak Hazukay, Fezza Mulalo Seguja alikuwa afisa wa ngazi za juu zaidi wa ADF na ndie alikuwa anaongoza mashambulizi ya ADF katika sekta ya Ruwenzori na eneo la kusini mwa Beni. 

Soma Zaidi: ADF yafanya mashambulizi mapya Kongo

Wakati wakaazi wa eneo hili wakililaumu jeshi kuwa na uzembe katika operesheni dhidi yaa ADF, msemaji wa jeshi kwenye Sekta ya operesheni Sokola1 Grand Nord kapteni Anthony Mualushayi alisema, kwamba katika vita dhidi ya magaidi, kunakushinda na kushindwa, lakini hilo haliwezi kwamwe kukatisha tamaa jeshi pamoja na raia. 

"Wakati tunapigana na magaidi wa ADF-MTM tunawezakushinda vita leo na kesho tunawezakushindwa vita na hiyo haiwezitupelekea kulegeza kamba. Tunachokiomba kwa raia wetu nikutokata tamaa kwani hayo ndio malengo ya magaidi, kutuvunja moyo, kufanya ukatili, na kusabisha woga ili wakaazi wavitoroke vijiji husika ili wao wavitawale na kuzindisha mauwaji pamoja na mashambulizi," alisema.

Kundi la Allied Democratric Forces - ADF, linalojiita Dola la Kiislamu linadai kuwa tawi lake la Afrika ya Kati, ni mmoja na makundi katili zaidi mashariki mwa Kongo, likituhumiwa kuwachinja maelfu ya raia.

Soma Zaidi:Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuitembelea DRCongo huku vurugu zikiendelea 

John Kanyunyu- Beni