1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yasema imedungua droni ya Ukraine iliyoelekezwa Moscow

31 Agosti 2023

Meya wa Moscow Sergei Sobyanin, amesema ndege moja isiyokuwa na rubani ya Ukraine imedunguliwa kupitia mfumo wa ulinzi wa angani wa Urusi, ilipovurumishwa kuelekea mjini Moscow.

https://p.dw.com/p/4VnWw
Russland I Moskau Bürgermeister Sergei Sobyanin
Picha: Mikhail Metzel/Sputnik/AP/picture alliance

Sobyanin amesema hakuna mali iliyoharibiwa au watu kujeruhiwa katika tukio hilo

Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema droni hiyo ilidunguliwa kusini Mashariki mwa mji wa Moscow katika wilaya ya Voskresensky. Vyombo vya habari vya Urusi vimeripoti ucheleweshwaji wa safari za ndege katika viwanja vya ndege mjini humo kufuatia tukio hilo.

Katika siku za hivi karibuni ndege zimekuwa na changamoto ya kupaa na kutua katika viwanja hivyo kufuatia kitisho kinachotolewa na ndege zisizokuwa na rubani kurushwa upande wa Urusi. 

Mashambulizi ya droni ya Ukraine dhidi ya Moscow yanaweza kuongezeka

Ukraine imekuwa ikiimarisha kujibu mashambulizi ya Urusi kupitia ndege hizo. Droni kadhaa zilielekezwa Magharibi mwa Urusi na baadhi zikaulenga uwanja wa ndege wa Pskov unaopakana na Latvia na Estonia na pia kuharibu ndege mbili za kijeshi za Urusi.

Ukraine inajaribu kujilinda dhidi ya miezi 18 ya uvamizi kikamilifu wa kijeshi kutoka kwa jirani yake Urusi, uliosababisha mauaji mengi pamoja na uharibifu mkubwa wa miundombinu yake. 

Urusi yasema itajibu mashambulizi dhidi yake

Droni ya Ukraine ikiwa angani Druzhkivka
Droni ya Ukraine ikiwa angani DruzhkivkaPicha: Wolfgang Schwan/AA/picture alliance

Kulingana na wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi, mashambulizi yanayofanywa dhidi yake yatajibiwa na kuongeza kuwa droni zinazotumika zisingeweza kufika mbali na kuingia nchini Urusi bila ya usaidizi wa Mataifa ya Magharibi. 

Mataifa hayo yameitaka Ukraine kutotumia silaha wanazoipa kushambulia ndani ya Urusi lakini wakati huo huo yakasema pia Kiev ina haki ya kujilinda na kufanya mashambulizi hayo ikitumia silaha zake na sio zile za msaada. 

Urusi yazuia mashambulizi kadhaa ya ndege zisizokuwa na rubani za Ukraine

Katika tukio tofauti jeshi la Ukraine limesema wanajeshi wake sita waliuwawa siku ya jumanne baada ya ndege zake mbili kuanguka karibu na mji wa Bakhmut Mashariki mwa taifa hilo. Halikutoa taarifa zaidi ya kile kilichotokea lakini limesema wote waliouwawa walikuwa maafisa wake.

Huku hayo yakiarifiwa vidio mpya iliyotolewa inamuonesha kiongozi wa kampuni ya wapiganaji binafsi wa Urusi wagner, Yevgeny Prigozhin akizungumza kuhusiana na hali yake na kitisho cha usalama wake.

Vidio yazuka ikimuonyesha Yevgeny akisema yuko salama siku kadhaa kabla ya kifo chake 

Vidio hiyo inayomuonyesha Prighozin akiwa Afrika siku chache kabla ya kifo chake na akiwahakikishia wale aliyodai wanataka kumuua, au kujua zaidi kuhusu maisha yake binafsi kwamba yuko salama. 

Kiongozi wa kundi binafsi la wapiganaji la Urusi Wagner Yevgeny Prigozhin
Kiongozi wa kundi binafsi la wapiganaji la Urusi Wagner Yevgeny Prigozhin Picha: Stringer/AFP

Vipimo vya DNA vyathibitisha kifo cha Prigozhin

Vidio hii iliyotolewa na mtandao wa Grey Zone wa Telegram ulio na mafungamano na kundi la Wagner, haikuweza kuthibitishwa na shirika la habari la Reuters mahali aliko au tarehe ilipochukuliwa lakini matamshi yake yanaonesha kuwa alikuwa anajua kwamba yuko hatarini.  

Yevgeny Prigozhin na wenzake 10 waliuwawa katika ajali ya ndege iliyotokea Kaskazini mwa Urusi tarehe 23 mwezi Agosti. Alizikwa katika makaburi ya Porokhovskoye katika mji wa St Petersburg. Urusi imekanusha madai ya nchi za Magharibi kwamba rais Putin amehusika na kifo chake. 

afp/ap/reuters