1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi yaanza mfululizo wa mashambulizi dhidi ya Ukraine

16 Desemba 2022

Msemaji wa jeshi la angani la Ukraine Yurii Inhat, amesema Urusi imefyatua zaidi ya makombora 60 Ijumaa dhidi ya miji kadhaa ya Ukraine ikiwa ni msururu wa mashambulizi mapya ya angani.

https://p.dw.com/p/4L2tz
Ukraine - Zerstörung in Vyshgorod vor Kiew nach russischem Luftangriff
Picha: Efrem Lukatsky/AP

Maafisa nchini Ukraine wameripoti kwamba Urusi imefanya mashambulizi katika miji mitatu ukiwemo mji mkuu Kiev kulenga vituo vya nishati na miundombinu mingine.

Imeripotiwa kwamba tayari mashambulizi hayo makubwa yameathiri mfumo wa usambazaji maji mjini Kiev. 

Ulaya yaidhinisha vikwazo vipya dhidi ya Urusi kutokana na kuivamia Ukraine

Msemaji wa jeshi la angani la Ukraine Yurii Inhat, amesema Urusi imefyatua zaidi ya makombora 60 leo dhidi ya miji kadhaa ya Ukraine ikiwa ni msururu wa mashambulizi mapya ya angani.

Watu wawili wameripotiwa kuuawa kufuatia shambulizi la roketi dhidi ya makaazi ya watu katika mji wa kusini Kryvyi Rig na wengine watano wamejeruhiwa wakiwemo watoto wawili. Hayo ni kwa mujibu wa meya wa mji huo Valentyn Reznichenko.

Urusi yaendelea kushambulia miji ya Ukraine kwa makombora

Miji kadhaa yakosa umeme kufuatia mashambulizi mapya

Kulingana na maafisa nchini Ukraine, miji ambayo imelengwa kwenye mfululizo huo wa mashambulizi ni pamoja na mji mkuu Kiev, mji wa kusini Kryvy Rig, na mji wa Kaskazini-mashariki Kharkiv.

Scholz: Ulaya na Ujerumani zimeungana kuisaidia Ukraine

Meya wa Kharkiv Ihor Terekhov amesema kupitia ukurasa wake wa Telegram kwamba mji wake hauna umeme. Gavana wa jimbo la Kharkiv Oleh Syniehuboy ameripoti kwamba mashambulizi matatu yalifanywa dhidi ya miundombinu mitatu ambayo ni muhimu kwa mji huo.

Kyrylo Tymoshenko, afisa wa ngazi ya juu katika ikulu ya Rais Volodymyr Zelensky pia ameripoti kwamba shambulizi moja lililenga jengo la wakaazi katika mji wa Kryvyi Rih. Kupitia ukurasa wake wa Telegram, ametahadharisha kwamba huenda kuna watu wamefunikwa kwenye vifusi vya jengo hilo lililoporomoka baada ya kushambuliwa. Waokoaji wanaendelea kufukua vifusi hivyo.

Jeshi la angani la Ukraine limesema Urusi imefyatua zaidi ya makombora 60 leo dhidi ya miji kadhaa ya Ukraine.
Jeshi la angani la Ukraine limesema Urusi imefyatua zaidi ya makombora 60 leo dhidi ya miji kadhaa ya Ukraine.Picha: Gleb Garanish/REUTERS

Wakaazi washauriwa kutafuta maeneo salama

Naye meya wa mji mkuu Kiev Vitali Klitschko, ameripoti kwamba zaidi ya wilaya nne za mji huo zimeshambuliwa. Amewataka wakaazi kutafuta maeneo salama.

Marekani kuipa Ukraine mfumo wa Patriot, Urusi yasema ni uchokozi

Ameandika kwenye ukurasa wake wa Telegram kwamba "mashambulizi dhidi ya mji mkuu yanaendelea. Huduma za usafiri wa reli zimesitishwa katika mji huo. Amesema hayo huku baadhi ya wakaazi wa mji huo wakikimbilia njia za chini ya ardhi za treni kujificha dhidi ya mashambulizi.

Kwa mara ya kwanza mji mkuu Kiev ulielekezewa makombora mengi zaidi kuwahi shuhudiwa tangu mwanzo ya uvamizi huo Februari 24. Takriban makombora 40 yamerekodiwa katika anga ya mji huo. Hayo ni kulingana na taarifa ya maafisa wa mji huo. Taarifa hiyo imeongeza kuwa kati ya makombora hayo, 37 yaliharibiwa na mfumo wa ulinzi wa angani.

Kampuni ya taifa inayosimamia reli nchini Ukraine Ukrzaliznytsia imesema umeme umekatika katika vituo vingi vya treni mashariki na maeneo ya kati mjini Kharkiv, maeneo ya Kirovohrad, Donetsk na Dnipropetrovsk kufuatia mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati. Hata hivyo katika maeneo mengine, treni zimeendelea kuhudumu kwa kubadili mifumo yao, kuachana na injini ya umeme na kutumia injini au mitambo inayoendeshwa na mvuke.

Kwa nini Urusi inashambulia miundombinu ya nishati Ukraine?

Urusi imekuwa ikishambulia miundombinu ya nishati ya Ukraine ili kuwatumbukiza kwenye baridi hali wanayofikiri itawalazimisha kusalimu amri msimu huu wa baridi kali.
Urusi imekuwa ikishambulia miundombinu ya nishati ya Ukraine ili kuwatumbukiza kwenye baridi hali wanayofikiri itawalazimisha kusalimu amri msimu huu wa baridi kali.Picha: Ed Ram/Getty Images

Mashambulizi kama hayo dhidi ya miundombinu ya nishati, yamekuwa sehemu ya mkakati mpya wa Urusi kujaribu kuwatumbukiza raia wa Ukraine katika hali ngumu majira haya ya baridi kali ili wasalimu amri. Hii ni baada ya vikosi vyake vya jeshi kushindwa kwenye maeneo muhimu ya mapambano katika miezi ya hivi karibuni.

Putin asema Urusi iko tayari kwa makubaliano na Ukraine

Lakini baadhi ya wachambuzi na viongozi wa Ukraine wanasema mashambulizi mapya ya Urusi yanaimarisha zaidi azimio la raia wa Ukraine kupambana dhidi ya uvamizi huo wa Urusi ulioanza Februari 24.

Mfululizo wa mashambulizi kama hayo ya Urusi dhidi ya miji ya Ukraine, awali ulifanyika Disemba 5. Maafisa wa Ukraine wameripoti kufanikiwa kuzuia au kuharibu baadhi ya makombora, roketi na ndege za mashambulizi zisizokuwa na marubani yaani drones za Urusi.

Umoja wa Ulaya wapitisha vikwazo vipya dhidi ya Urusi

Vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya vitalenga viwanda vya kijeshi pamoja na watu au mashirika yanayohusishwa na mashambulizi dhidi ya raia Ukraine.
Vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya vitalenga viwanda vya kijeshi pamoja na watu au mashirika yanayohusishwa na mashambulizi dhidi ya raia Ukraine.Picha: Olivier Matthys/AP/picture alliance

Umoja wa Ulaya umesema vikwazo vyake vipya vitalenga viwanda vya silaha za kijeshi vya Urusi, watu na makundi ambayo yanashambulia raia wa Ukraine au wanaowateka nyara watoto wa Ukraine. Kauli hiyo imejiri mnamo wakati Urusi imeanzisha mfululizo wa mashambulizi mapya dhidi ya Ukraine.

Valdis Dombrovskis, naibu rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya amesema vikwazo hivyo 168, vitalenga kampuni, mashirika ya serikali na vilevile watu maalum.

Vikwazo hivyo vya tisa, ambavyo ni adhabu za Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi kufuatia vita vyake nchini Ukraine, viliidhinishwa na viongozi wa umoja huo Alhamisi na kupitishwa rasmi Ijumaa.

Mkuu wa halmashauri kuu ya umoja huo Ursula von der Leyen, amesema vikwazo hivyo vitalenga pia sekta ya teknolojia, fedha na vyombo vya Habari nchini humo, kuubana uchumi wa Urusi na kukandamiza operesheni zake za vita.

Kulingana na Von der Leyen, takriban watu 200 na mashirika yanayohusishwa na mashambulizi dhidi ya raia na kuwateka watoto nyara wanalengwa na vikwazo hivyo.
Vyanzo:(APE,AFPE,RTRE)

Tafsiri: John Juma

Mhariri: Daniel Gakuba