1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi: Malengo ya vita Ukraine yazidi mazungumzo ya amani

28 Februari 2023

Serikali ya Urusi imesema malengo ya vita vya Ukraine yana umuhimu zaidi kuliko uwezekano wowote wa mazungumzo ya amani.

https://p.dw.com/p/4O58D
Russland | Dmitri Peskow
Picha: Sergei Savostyanov/TASS/dpa/picture alliance

Msemaji wa serikali ya Urusi Dmitry Peskov, amesema hadi sasa hakuna ishara kutoka Ukraine kwamba wako tayari kushiriki mazungumzo. Ameongeza kwamba katika hali hiyo, kutimiza malengo yao ndiyo hatua muhimu zaidi kwao, na ndicho kipaumbele chao.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alikataa mazungumzo na Rais wa Urusi Vladimir Putin na mara kadhaa mmependekeza mpango wake mwenyewe unaosema sharti Urusi kwanza iondoe vikosi vyake vyote nchini Ukraine ndipo kuwe na mazungumzo yoyote ya amani.

Guterres: Haki za binaadamu zinadhoofishwa na vita

Urusi ambayo ilianzisha uvamizi nchini Ukraine mwaka mmoja uliopita imekataa pendekezo hilo inalosema ni upuuzi.

Peskov amesema kwamba kabla ya mazungumzo yoyote, ni sharti Ukraine iyatambue majimbo manne ya Donetsk, Luhansk, Zaporizhzhya na Kherson sasa ni sehemu ya Urusi kikatiba. Amesema huo ndio uhalisia wa mambo ambao ni muhimu.

Hata hivyo Urusi bado haina udhibiti kamili wa majimbo hayo iliyoyachukua kutoka Ukraine kwa kukiuka sheria ya kimataifa.

Ukraine yasema hali ya vita ni ngumu Bakhmut

Ukraine yasema hali ni ngumu katika mji wa Bakhmut ambako mashambulizi makali yanaendelea.
Ukraine yasema hali ni ngumu katika mji wa Bakhmut ambako mashambulizi makali yanaendelea.Picha: Jose Colon/AA/picture alliance

Peskov amesema pia kuwa lengo lao jingine ni kutaka kuondolewa kwa jeshi la Ukraine ambalo limekuwa likipewa silaha na nchi za Magharibi.

Kwenye mazungumzo na gazeti linalopendelea Urusi la Izyestia, chapisho la Jumanne, Peskov alisema mengi yamesemwa na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuhusu vita vya Ukraine, lakini hakuna hatua ambazo zimechukuliwa kutoka upande wao kujaribu kutoa suluhisho.

Kando na hayo, jeshi la Ukraine lilisema hapo awali Urusi iliimarisha vikosi vyake katika eneo la Bakhmut na ilikuwa ikishambulia kwa makombora karibu na mji huo.

Urusi imesema vikosi vyake vimeharibu ghala la kuhifadhia risasi la Ukraine karibu na mji wa Bakhmut na kuangusha roketi zilizotengenezwa na Marekani na ndege zisizo na rubani za Ukraine, ripoti ambazo hazikuweza kuthibitishwa na vyanzo huru. 

Stoltenberg azidisha wito kutaka Sweden na Finland kuruhusiwa katika NATO

Jens Stoltenberg azihimiza Uturuki na Hungary kuridhia Sweden na Finland kuwa wanachama wa jumuiya ya kijeshi ya NATO.
Jens Stoltenberg azihimiza Uturuki na Hungary kuridhia Sweden na Finland kuwa wanachama wa jumuiya ya kijeshi ya NATO.Picha: Heikki Saukkomaa/picture alliance/dpa/Lehtikuva

Katika tukio jingine, mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesisitiza wito wake kwa Uturuki na Hungary kuruhusu Finland na Sweden kujiunga na jumuiya hiyo ya kijeshi ya nchi za Magharibi.

EU yakubali kuiwekea Urusi vikwazo zaidi

"Muda umetimia wa kuidhinisha kikamilifu na kuzikaribisha Finland na Sweden kama wanachama," Stoltenberg alisema hayo akiwa Helsinki akiwa na waziri mkuu wa Finland Sanna Marin.

Ameongeza kuwa hatua zimepigwa mbele na Uturuki kuhusiana na suala hilo na kwamba mkutano umepangwa kufanyika wiki ijayo mjini Brussels kati ya wawakilishi wa Ankara, Stockholm na Helsinki.

Nchi hizo mbili za kaskazini mwa Ulaya na kaskazini mwa Atlantiki, zilituma maombi ya kujiunga na jumuiya ya kijeshi ya NATO mwezi Mei mwaka uliopita kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Hata hivyo, maombi yao sharti yaidhinishwe na nchi zote wanachama wa NATO. Uturuki na Hungary hazijaridhia maombo hayo.

(Vyanzo: DPAE)