1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine yasema hali ni ngumu sana katika mji wa Bakhmut

28 Februari 2023

Kamanda wa vikosi vya ardhini vya Ukraine amesema hali ni ngumu sana katika mji wa Bakhmut Jumanne (28.02.2023) wakati vikosi vya Urusi vikiongeza mashambulizi katika jaribio la kuuzingira kikamilifu

https://p.dw.com/p/4O4VL
Ukraine Krieg | Ukrainische Soldaten in Soledar
Picha: Roman Chop/AP Photo/picture alliance

Kamanda huyo Jenerali Oleksandr Syrskyi amenukuliwa akisema kwenye jukwaa la kijeshi la mtandao wa Telegram kwamba licha ya haraka kubwa, adui ametumia vikosi vilivyojiandaa zaidi vya mashambulizi kutoka kundi la mamluki la Wagner, vinavyojaribu kuvunja ngome za majeshi ya Ukraine na kuuzingira mji wa Bakhmut. Rais Volodymyr Zelenskiy pia alisema jana Jumatatu kwamba adui yao anaharibu kila kitu kinachoweza kutumia kulinda ngome zao, na kuwataja wanajeshi wanaotetea eneo la karibu na Bakhmut kuwa mashujaa wa kweli.

Zelensky asema wanahitaji sehemu ya ndege kwenye mfumo wa ulinzi wa anga

Zelenskiy ameongeza kusema kwamba ndio maana, kwa sababu ya mashambulizi kama hayo, wanahitaji sehemu ya ndege kwenye mfumo wa ulinzi wa anga, ndege za kisasa za kivita ili kulinda eneo lote la nchi yao dhidi ya ugaidi wa Urusi.  Jeshi la Ukraine lilisema hapo awali Urusi iliimarisha vikosi vyake katika eneo la Bakhmut na ilikuwa ikishambulia kwa makombora karibu na mji huo. Wanajeshi wa Ukraine katika mkoa wa Donetsk walijificha kwenye mitaro ya matope baada ya hali ya hewa ya joto kulainisha ghafla ardhi iliyoganda.

Ukraine Tschassiw Jar | Zerstörte Gebäude
Mji wa Bakhmut nchini UkrainePicha: Jose Colon/AA/picture alliance

Urusi imesema kuwa vikosi vyake vimeharibu ghala la kuhifadhia risasi la Ukraine karibu na Bakhmut

Mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa Ukraine Oleh Zhdanov amesema vikosi vya Urusi vimesababisha matatizo kati ya vijiji hivyo wakati vikijaribu kuzuwia barabara ya magharibi kuelekea Chasiv Yar. Urusi ilisema kuwa vikosi vyake vimeharibu ghala la kuhifadhia risasi la Ukraine karibu na Bakhmut na kuangusha roketi zilizotengenezwa na Marekani na ndege zisizo na rubani za Ukraine, ripoti ambazo hazikuweza kuthibitishwa na vyanzo huru.  Wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema Marekani inapanga uchochezi nchini Ukraine kwa kutumia kemikali za sumu. Hakukuwa na jibu la mara kutoka Marekani kuhusiana na madai hayo.

Msaada zaidi waahidiwa kwa Ukraine

Mjini Kyiv, waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen alikuwa afisa mwandamizi wa karibuni zaidi kutoka magharibi kuuzuru mji huo mkuu wa Ukraine, na kuahidi msaada na hatua zaidi za kuitenga Urusi, baada ya kukutana na Rais Volodymyr Zelenskiy na mataifa wengine. Bosi wake, Rais Joe Biden, alikwenda huko wiki moja iliyopita kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka wa kwanza wa uvamizi wa Urusi. Mjini Astana, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, ameahidi msaada wa Marekani kwa ajili ya uhuru wa Kaskakhstan akiwa katika ziara ya kuimarisha katika kanda ya Asia ya Kati, ambayo imetikiswa pia na uvamizi wa Urusi Ukraine.