1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Venezuela kuandamana kupinga matokeo

Hawa Bihoga
2 Agosti 2024

Kiongozi wa Upinzani nchini Venezuela, Maria Corina Machado, ameitisha maandamano makubwa kuanzia kesho Jumamosi kulaani na kupinga kile alichokiita kuchaguliwa tena kwa Rais Nicolas Maduro.

https://p.dw.com/p/4j2D3
Venezuela l Siasa l Maria Corina Machado.
Kiongozi wa upinzani Venezuela Maria Corina Machado akizungumza na wafuasi wake wa kisiasa.Picha: Jeampier Arguinzones/dpa/picture alliance

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Machado aliwahimiza wafuasi wake ambao tayari wameingia mitaani kuandamana wakipinga matokeo hayo kwamba lazima wabaki imara na kuwa na mwamko wa kudai ushindi.

Aidha mapema hapo jana kupitia jarida la Wall Street aliandika kwamba yupo mafichoni na anahofia kile alichokiita usalama wa maisha yake baada ya ushindi wa Maduro, ambao ulisababisha mamia ya watu kukamatwa kufuatia maandamano ya juma hili.

Alisema mbali na maandamano hayo kupinga ushindi wa Maduro lakini pia yataonesha uungwaji mkono kwa watu ambao wamewekwa kizuizini kufuatia kupinga ushindi wa Maduro.

Katika ujumbe kwa njia ya video , Machado alirejelea msimamo wao kwamba upinzani ulishinda uchaguzi na kusema 'watabaki imara'.

"Kila mchapakazi anayetaka kuishi kwa utu na haki alishinda. Kila kijana ambaye hataki kuondoka au ambaye anataka kurudi katika nchi yake alishinda. Sote tumeshinda, " Alisema hotuba yake ambayo pia ilipeperushwa na wafuasi wake kupitia mitandao ya kijamii

"Sasa tunaenda kuchukua ushindi wetu. Ni lazima tuwe imara, tujipange na kuhamasishana."

Soma pia:Upinzani wawataka Wavenezuela kumpinga Maduro

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa upinzani, takriban watu 20 waliuwawa kufuatia maandamano ya kupinga ushindi wa Maduro ambao ulipongezwa na washirika wake wa karibu ikiwemo China, huku wengine zaidi 1,000 wakikamatwa.

Mahamahaka ya Juu Venezuela imewaita wagombea wote wa uarais leo Ijumaa mchana kufuatia ombi la Rais Maduro la kutaka ianzishe mchakato wa kuchunguza na kuthibitisha matokeo ya uchaguzi huo unaotajwa kujaa udanganyifu.

Taifa hilo la Amerika ya Kusini lilitumbukia kwenye mzozo wa kisiasa baada ya Rais Maduro kutangazwa tena mshindi katika matokeo ya uchaguzi siku ya Jumapili, matokeo ambayo yalikinzana na kura za maoni kabla ya uchaguzi  na kuibua ukosoaji mkubwa wa kimataifa.

Marekani: Kuna ushahidi Gonzalez alishinda

Marekani, ambayo ina maslahi makubwa kwenye uchimbaji mafuta nchini Venezuela, hapo jana ilidai kwamba "kuna ushahidi wa kutosha" kwamba mgombea wa upinzani ambaye ni mwanadiplomasia wa zamani, Edmundo Gonzalez, alishinda katika uchaguzi huo ambao tume ya uchaguzi ilimtangaza Maduro kuwa mshindi licha ya kuenea kwa madai ya ulaghai.

Venezuela Uchaguzi 2024 | Siasa | Nicolas Maduro na Edmundo Gonzalez Urrutia
Rais wa Venezuela Nicolas Maduro na Mgombea urais wa upinzani Edmundo Gonzalez Urrutia.Picha: Yuri Cortez/AFP/Rances Mattey/Anadolu/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken alikwenda mbali zaidi na kumpongeza mwanasiasa huyo wa upinzani Gonzalez, kwa kile alichokiita "kampeni za uchaguzi zenye mafanikio"

Katika tamko lake Blinken alivitaka vyama vya upinzani nchini Venezuela kuanza kujadiliana makabidhiano ya madaraka kwa njia ya heshima na amani kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi Venezuela na matakwa ya watu wake na kusisitiza kwamba Maduro anapaswa kukubali ushindi wa Gonzalez.

Soma pia:Upinzani Venezuela watafuta njia ya kuingia madarakani

Brazil, Mexico na Colombia ambazo marais wake wamekuwa na ukuruba na Rais Maduro wameitaka tume ya uchaguzi Venezuela kuweka hadharani matokeo ya uchaguzi na kuongeza kwamba wanayo nia ya kuunga mkono juhudi za mazungumzo na kutafuta makubaliano ambayo yatawanufaisha Wavenezuela.

Katika kukabiliana na ukosoaji unaohusiana na uchaguzi, Venezuela imewafukuza wanadiplomasia wa Argentina na nchi nyingine tano ikiwemo Chile, Costa Rica, Panama, Jamhuri ya Dominika na Uruguay.