1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtu mmoja amekufa katika maandamano ya Venezuela

Sylvia Mwehozi
30 Julai 2024

Mtu mmoja amefariki katika maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi nchini Venezuela huku maandamano zaidi yakitarajiwa kufanyika leo Jumanne.

https://p.dw.com/p/4iu6J
Maandamano ya Venezuela
Waandamanaji wakikabiliana na vikosi vya usalamaPicha: YURI CORTEZ/AFP via Getty Images

Shirika moja lisilo la kiserikali la Foro Penal, ndio limethibitisha kifo cha mtu mmoja kupitia mtandao wa X na kusema kwamba mtu huyo amefariki katika jimbo la kaskazini la Yaracuy, ingawa maelezo zaidi hayakujulikana hapo awali. Vyombo vya habari vya nchini humo vimeripoti vifo vya watu wawili.

Maandamano hayo ya nchi nzima yamefanyika jana Jumatatu kufuatia uchaguzi wenye utata ambao umempatia muhula mwingine rais Nicolas Maduro na kusababisha makabiliano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama. Picha za vidio zilizorushwa na televisheni za nchini humo zimewaonyesha polisi wakitumia gesi ya kutoa machozi na kuwakamata baadhi ya waandamanaji. Polisi pia walifyatua risasi za moto dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakielekea katika ikulu ya rais kwenye mji mkuu wa Caracas.

Venezuela | Upinzani
Kiongozi wa upinzani wa Venezuela aliyeshika mic Maria Corina Machado karibu na mgombea wa upinzani wa upinzani Edmundo GonzalezPicha: Leonardo Fernandez Viloria/REUTERS

Upinzani umeitisha maandamano makubwa dhidi ya serikali leo Jumanne, lakini kambi ya serikali nayo imepanga kuandamana mitaani. Tume ya taifa ya uchaguzi ilimtangaza rasmi Maduro, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2013, kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais kwa asilimia 51.2ya kura katika uchaguzi uliofanyika Jumapili. Tume hiyo ilisema mgombea wa upinzani Edmundo Gonzalez aliibuka na asilimia 44.2 ya kura na upinzani umekataa kuyatambua matokeo hayo rasmi ukisema kulikuwa na udanganyifu.

Hapo jana, Gonzalez na kiongozi wa upinzani Maria Corina Machado waliwaeleza waandishi wa habari kwamba mgombea wao alijizolea zaidi ya asilimia 70 ya kura katika uchaguzi huo. Soma: Venezuela: Upinzani wapinga matokeo ya liompa ushindi Maduro

Akizungumza kuhusu ghasia hizo, Maduro amesema vikosi vya usalama vinaendelea kukabiliana na kile alichokitaja kuwa ni maandamano ya vurugu.

Maandamano ya Venezuela
Waandamanaji wakikanyaga bango la kampeni la MaduroPicha: RAUL ARBOLEDA/AFP via Getty Images

"Tumeshuhudia kundi linalofanya matukio ya vurugu. Sasa hivi naweza kukuonyesha video 100 za mashambulizi ya kikatili, tunaweza kuzitaja kuwa ni uhalifu na za kigaidi,” alisema Rais Maduro katika hotuba yake. 

Serikali ya Marekani na nchi kadhaa za Amerika ya Kusini pia walionyesha mashaka juu ya matokeo rasmi ya uchaguzi. Maduro anatazamiwa kuanza muhula wake wa tatu wa miaka sita ifikapo Januari 2025. Venezuela inakabiliwa na usimamizi mbovu wa serikali, rushwa na vikwazo vya kimataifa.

Zaidi ya asilimia 80 ya Wavenezuela wanaishi chini ya mstari wa umaskini. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa, zaidi ya watu milioni 7, karibu robo ya wakaazi wameondoka katika nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta katika miaka ya hivi karibuni kutokana na umaskini na ghasia.