1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan Kusini

Unyanyasaji dhidi ya wafanyakazi wa misaada umeongezeka

17 Agosti 2023

Umoja wa Mataifa umesema kwamba jumla ya wafanyakazi 62 ​​wa mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu wamefariki dunia mwaka huu duniani kote.

https://p.dw.com/p/4VI1v
Südsudan UN Friedensmission/Symbolbild
Picha: Ashraf Shazly/AFP

Wakati umoja huo ukijiandaa kuadhimisha miaka 20 tangu shambulio baya kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Baghdad. 

Umoja wa Mataifa huadhimisha Siku ya Misaada ya Kibinadamu Duniani ifikapo Agosti 19 kila mwaka huku ikikumbuka shambulio la bomu la kujitoa mhanga lililogharimu maisha ya watu 22, akiwemo Sergio Vieira de Mello, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu wakati huo na mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Baghdad.

Soma pia: Guterres asema MONUSCO inakaribia kuondoka Kongo

Kwa mujibu wa Hifadhi ya data ya Usalama wa Wafanyakazi wa Misaada iliyoandaliwa na kampuni ya ushauri ya Humanitarian Outcomes mbali na vifo 62 vilivyosajiliwa mwaka huu katika maeneo yenye mizozo duniani, wafanyakazi wengine 84 wa kutoa misaada walijeruhiwa na 34 walitekwa nyara. Idadi ya waliofariki kwa mwaka wote wa 2022 ilifikia watu 116.

Mataifa hatari kwa watoa misaada

Sudan Nord-Kordofan Lastwagen mit humanitärer Hilfe des Welternährungsprogramms (WFP) für südsudanesische Flüchtlinge
Msafara wa malori ya msaada wa chakula uliotolewa na Shirika la Mpango wa Chakula(WFP) Sudan KaskaziniPicha: ASHRAF SHAZLY/AFP

Kwa miaka kadhaa Sudan Kusini imekuwa sehemu hatari zaidi duniani kwa wafanyakazi wa misaada. Huku Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ikisema kwamba kufikia Agosti 10, kumekuwa na mashambulizi 40 dhidi ya wafanyakazi wa kibinadamu huko, huku watu 22 wakipoteza maisha.

Soma pia: Mapigano ya Sudan yanazidi kulididimiza taifa hilo

Inayofuata katika orodha hiyo ilikuwa Sudan kaskazini, kwa mashambulizi 17 na vifo 19 dhidi ya wafanyakazi wa misaada hadi sasa mwaka huu. Takwimu hizo ni rekodi ya juu ambayo haijaonekana tangu mzozo wa Darfur ulipoanzia 2006 hadi 2009.

Nchi nyingine ambapo wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu walifariki ni pamoja na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali, Somalia, Ukraine na Yemen.

Takwimu za wanaofariki

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Usalama lisilo la kiserikali, kila mwaka zaidi ya asilimia 90 ya watu wanaokufa katika mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa misaada ni wenyeji na mwaka huu Siku ya Kibinadamu Duniani inaadhimisha miaka 20 tangu shambulizi la bomu mjini Baghdad katika Hoteli ya Canal, ambayo ilikuwa makao makuu ya Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa Iraq.

Shambulizi hilo la mwaka 2003, lilitekelezwa katikati ya machafuko ya uvamizi ulioongozwa na Marekani ambao ulimwondoa madarakani Saddam Hussein, na kuwauwa watu 22, na kuwajeruhi takriban wafanyakazi 150 wa misaada wa ndani na kimataifa.

Huku misukosuko ikiongezeka kote ulimwenguni, Umoja wa Mataifa umesema unafanya kazi kuwasaidia karibu watu milioni 250 wanaoishi katika maeneo yenye matatizo. Hiyo ni mara 10 zaidi ya mwaka 2003.

Tazama pia: 

Miaka 70 ya mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu