1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa UN kupunguza taka za plastiki kwa 80% ifikapo 2040

17 Mei 2023

Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP) umesema katika ripoti yake kwamba mataifa yote ulimwenguni yanaweza kupunguza uchafuzi wa plastiki kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2040, ikiwa yatatumia teknolojia zilizopo.

https://p.dw.com/p/4RVrK
Kenia | Skulptur aus Plastikmüll
Picha: Brian Inganga/AP Photo/picture alliance

 Shirika hilo la Umoja wa Mataifa lenye makao yake nchini Kenya limefafanua sera zinazoweza kutumiwa ili kushughulikia mzozo wa taka za plastiki, wiki mbili kabla wajumbe kutoka nchi mbalimbali kukutana mjini Paris nchini Ufaransa kwa duru ya pili ya mazungumzo ya kuandaa mkataba wa kimataifa unaolenga kutokomeza taka za plastiki.

Ripoti hiyo inazingatia mabadiliko matatu muhimu ya soko hilo la plastiki ambayo yanahitajika kuunda uchumi unaofahamika kama wa "mduara" ambao hudumisha bidhaa zinazozalishwa katika mzunguko kwa muda mrefu iwezekanavyo kwa kuzingatia hatua za kutumia tena, kuchakata na kuachana na plastiki katika ufungaji wa bidhaa na kuanza kutumia nyenzo mbadala.

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa siku ya Jumanne na ambayo inaonya kuwa miaka michache ijayo itakuwa katika hatari zaidi, inabaini kuwa ni lazima ulimwengu upunguze nusu ya plastiki zinazotumika mara moja na nyenzo zinazotupwa kirahisi ili kukomesha wimbi la uchafuzi wa mazingira.

Soma pia: Mifugo waangamia Kenya kwa kula mifuko ya plastiki

Wasiwasi unaongezeka kuhusu athari za plastiki, na taka za plastiki zilizopatikana kwenye kina kirefu kabisa cha bahari hadi juu ya Mlima Everest. Kwa wanadamu, chembechembe hizo za vipande vidogo vya plastiki vimegunduliwa katika damu, maziwa ya mama na hata kwenye mfuko wa uzazi.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini New York siku ya Jumanne, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric,  amesema, ripoti ya Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa kuhusu uchafuzi wa mazingira utokanao na plastiki unaweza kupungua kwa asilimia 80 na kusababisha akiba ya zaidi ya dola bilioni 300 kwa mwaka ikiwa nchi na makampuni yatafanya mabadiliko ya kina ya sera na soko kwa kutumia teknolojia zilizopo. Dujarric ameendelea kusema:

" Ripoti inapendekeza kwanza kuondoa plastiki zisizo za lazima ili kupunguza ukubwa wa tatizo, na kisha kuweka mfumo wa kutumia tena nyenzo hizo, uchakataji na utofautishaji wa bidhaa za plastiki. Ripoti hiyo pia inapendekeza njia za kukabiliana na urithi uliobaki wa uchafuzi wa plastiki. Maelezo hayo yanapatikana kwenye mtandao."

Uchafuzi wa plastiki hatari kwa mazingira

2019 Niederlande | The Ocean Cleanup startet Interceptor zur Sammlung von Plastikmüll in Flüssen
Taka za plastiki zinadiriki katika uchafuzi wa mazingiraPicha: COVER Images/ZUMA Wire/IMAGO

Ripoti hiyo imeweka wazi utafiti uliokadiria kuwa uchafuzi wa plastiki unaweza kuchangia asilimia 19 ya uzalishaji wa gesi chafu duniani ifikapo mwaka 2040.

Hilo kimsingi lingeuzuia ulimwengu kufikia ahadi yake ya Makubaliano ya mjini Paris ya kupunguza ongezeko la wastani wa joto kwenye uso wa sayari hadi nyuzi joto 1.5 juu ya kiwango cha kabla ya kuanza kwa enzi za viwanda.  

Inger Andersen, mkurugenzi mtendaji wa UNEP amesema jinsi tunavyozalisha, kutumia na kutupa plastiki kunachafua mifumo ya ikolojia, na kuleta hatari kwa afya ya binadamu na kuathiri pia hali ya hewa.

Soma pia: UN: Mkataba wa kupambana na uchafuzi wa mazingira waundwa

Mnamo mwaka 2020, takriban tani milioni 238 za taka kutoka kwa plastiki zinazotumiwa kwa muda mfupi kama vile vifungashio ambavyo huishia kwenye taka za manispaa, zilizalishwa ulimwenguni kote. Takriban nusu ya taka hizo zilishughulikiwa vibaya, hususan kutupwa au kuchomwa moto.

Ikiwa hakutofanyika mabadiliko makubwa, UNEP inatarajia kuwa taka za plastiki kwa mwaka zitaweza kufikia kiwango cha milimita 408 ifikapo mwaka 2040, ikiwa ni pamoja na milimita 380 za plastiki mpya zinazotokana na nishati ya mafuta. Hiyo inamaanisha kuwa milimita 227 za plastiki zitaishia kutupwa na kuharibu mazingira.

Ripoti hiyo ilibaini kuwa uchakataji ukiambatana na sera iliyo bora vinaweza kupunguza uchafuzi wa mazingira kwa asilimia tano. Hilo litafikiwa kwa kuondolewa ruzuku za mafuta na utekelezaji wa sheria za usanifu ili kurahisisha kushughulikia nyenzo zinazotumiwa. Asilimia nyingine 17 ya kupunguza uchafuzi huo inawezekana kwa kutafuta mbadala wa matumizi ya plastiki kwa kutumia nyenzo kama karatasi au vifaa vingine.