Mifugo waangamia Kenya kwa kula mifuko ya plastiki
10 Januari 2023Hali hiyo imehusishwa na makali ya kiangazi yanayoshuhudiwa jimboni humo kwa wakati huu na kulazimisha mifugo waliosalia kutegemea mifuko ya plastiki inayopatikana kiurahisi.
Wakati makali ya kiangazi yakiendelea kushuhudiwa katika jimbo hili la Marsabit,hofu imeanza kuwavaa wafugaji ambao mifugo yao imeanza kufariki baada ya kula mifuko ya plastiki.
Kwa mujibu wa Mzee Golloh Wario, mfugaji kutoka eneo bunge la Horr Kaskazini, kupungua kwa lishe ya mifugo kumewapelekea wafugaji wengi kuanza kuwalisha mifugo mifuko ya plastiki ambayo imeonekana kama suluhu ya muda.
Hata hivyo Mzee Wario anasema tayari madhara ya kuwapa mifugo plastiki hizo imeanza kuonekana wazi kutokana na idadi kubwa ya mifugo wanaoripotiwa kuangamia. "Nilikuwa na ng'ombe thelathini na kwa sasa nimesalia na wawili tu na kwa sababau wakati huu hakuna malisho,nalazimika kuwalisha mifuko ya plastiki…”
Kulingana na mwanamazingira wa hapa marsabit John Waqo Duba, ongezeko la mifuko ya plastiki limeendelea kuwa tishio kwa maisha ya mifugo na kuna haja ya serikali kuchukua hatua ya kudhibiti ongezeko hilo kabla ya hali kuwa mbaya Zaidi.
"Kwa sasa, mifugo hawana malisho na wafugaji wengi wanalazimika kuwapa mifugo waliosalia boksi. Hii inahatarisha Maisha yao”
Mifuko ya plastiki imeendelea kutumika Marsabit licha ya serikali kupiga marufuku matumizi yake nchini.
Mkurugenzi wa mamlaka ya mazingira katika jimbo la Marsabit Vincent Oloo anasema kuwa, matumizi ya mifuko ya plastiki imeendelea kuwa tishio na kwamba tayari washukiwa wanane wamekamatwa baada ya kupatikana wakiuza mifuko hiyo ambayo imeendelea kuhatarisha maisha ya binadamu na mifugo. Oloo amekiri kupokea ripoti za maafa ya mifugo walioripotiwa kula mifuko ya plastiki.
"Wakati mifugo wanapokula mifuko ya plastiki,huwa inachukuwa muda mrefu kabla ya mifuko hiyo kujisaga tumboni na hali hii husababisha madhara makubwa kwa mnyama n ahata ukitembelea vichinjio vya hapa Marsabit,utaona kwamba,wengi wa mifugo wanaochinjwa huwa na mifuko ya plastiki tumboni”
Oloo ameeleza kwamba, mamlaka ya mazingira, NEMA tayari imeanzisha uchunguzi kufuatia ripoti kwamba,baadhi ya kampuni zimekuwa zikitumia mifuko ya plastiki katika kupakia bidhaa zao mjini Marsabit na kuhatarisha maisha ya viumbe hai.
Jimbo la Marsabit limeendelea kuripoti hali mbaya ya kiangazi na kuwasukuma wafugaji kutafuta mbinu za kuwaokoa mifugo wao ikiwemo kuwalisha mifuko ya plastiki kwa wakati huu.
Michael Kwena, DW Marsabit