1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaomba amani, Urusi ikiishambulia Ukraine

29 Aprili 2022

Wizara ya ulinzi ya Urusi imethibitisha hii leo kwamba ilifanya shambulizi la angani katika mji wa Kyiv wakati katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa ziarani nchini Ukraine jana Alhamisi.

https://p.dw.com/p/4AbpC
Ukraine | Antonio Guterres in Irpin
Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Urusi inatoa taarifa hii baada ya hapo jana katibu mkuu huyo kutoa mwito wa kusitishwa kwa mashambulizi katika mkutano na waandishi wa habari akiambatana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky. 

Soma Zaidi: Milipuko katikati mwa mji wa Kyiv huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akifanya ziara nchini Ukraine.

Taarifa ya wizara hiyo ya ulinzi ya Urusi ambayo hutolewa kila siku kuhusiana na mzozo wa Ukraine imesema wanajeshi wake walifanya mashambulizi kadhaa ya anga siku ya Alhamisi na kuharibu vituo vitatu vya kusambaza nishati na baadhi ya majengo ya viwanda vya silaha nchini Ukraine. Ukraine imesema kwamba mtu mmoja aliuawawa kwenye shambulizi hilo la jana ambalo ni kwa kwanza katika mji wake mkuu Kyiv katika kipindi cha karibu wiki mbili na ambalo msemaji wa katibu mkuu Antonio Guterres amelielezea kama la kushtusha mno.

Guterres hapo jana aliutembelea mji wa Bucha na maeneo mengine ya Kyiv ambako inadai kwamba kulifanyika uhalifu wa kivita na kwenye mkutano na waandishi wa habari katibu mkuu huyo alitoa mwito wa kusitishwa kwa mapigano na kuanzishwa kwa mchakato wa amani kwa kuzingatia misingi ya mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.

"Hivi vita lazima vikomeshwe na kurejeshwa kwa amani kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria ya kimataifa"alisema Guterres.

Soma Zaidi: Guterres aitolea mwito Urusi kumaliza vita Ukraine

Ukraine Kiew | Pressekonferenz Antonio Guterres und Wolodymyr Selenskyj
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (kushoto) rais wa Urusi Volodymyr Zelensky, wkati katibu mkuu huyo alipotembelea Ukraine.Picha: Efrem Lukatsky/AP/picture alliance

Katika hatua nyingine, ofisi ya rais wa Ukraine imesema kwenye taarifa kwamba inaandaa operesheni ya kuwaondoa raia waliokwama katika eneo la viwanda lililozingirwa la Azovstal katika mji wa Mariupol. Tangazo hilo linatolewa siku moja baada ya Guterres kusema taasisi yake inafanya kila linalowezekana kuhakikisha raia takriban 100,000 wanaokabiliwa na kitisho kutokana na mashambulizi ya Urusi wanaokolewa kutoka katika mji huo.

Siku ya Jumanne, Guterres alipozungumza na rais wa Urusi Vladimir Putin walikubaliana kimsingi kuwaondoa raia hao wakiyahusisha mashirika ya ya kimataifa na Umoja wa Mataifa

Nchini Uingereza, waziri wa mambo ya kigeni Liz Truss amesema mapema leo kwamba watapeleka wataalamu kuisaidia Ukraine kukusanya vidhibiti na kufungua kesi ya uhalifu wa kivita katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC. Wataalamu hao wanatarajia kufika Poland mapema mwezi Mei. Ukraine inasema inachunguza takriban visa 7,600 vya uhalifu wa kivita na washukiwa wasiopungua 500 tangu uvamizi wa Urusi mwezi Februari 24.

Soma Zaidi:Macron, Scholz waepuka kutaja mauaji ya Ukraine kuwa "halaiki" 

Truss, ameongeza kuwa Urusi imefanya ukatili na uovu nchini Ukraine ikiwa ni pamoja na dhidi ya wanawake na waatalamu hao wa Uingereza watasaidia kuvumbua ukweli na kuiwajibisha serikali ya rais Putin kwa hatua zake. Tangazo hilo linatolewa wakati Truss akielekea The Hague akiongozana na waziri mwenzake wa Uholanzi Wopke Hoekstra kukutana na rais wa ICC Jaji Poitr Hofmanski.

Huko Tokyo kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amehitimisha ziara yake fupi nchini Japan hii leo kwa kutembelea mtambo wa Hydrogen katika mji mkuu Tokyo ikiwa ni sehemu ya kusaka vyanzo vipya vya nishati wakati Berlin ikijaribu kujiengua na utegemezi wa nishati kutoka kwa Urusi kutokana na vita hivyo vya Ukraine. Hapo jana Scholz alikutana na waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida na kukubaliana kuimarisha ushirikiano huku Kishida akiipongeza Ujerumani kwa hatua yake ya kupeleka silaha nzito nchini Ukraine.

Mashirika: RTRE/DW/DPAE